WIZARA ya Fedha imesema inatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma kuhusu sera, mipango na mikakati na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali kupitia wizara hiyo.
Akizungumza katika warsha ya wanahabari mtandao mjini Morogoro,Salome Kingdom Mchumi mkuu kutoka wizara ya Fedha amesema kuwa wametoa elimu kwa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii namna gani kuandika habari za kibajeti na habari za miradi mbalimbali.
Kingdom amesema kuwa wametoa mafunzo hayo kwa lengo la kuhakikisha waandishi wa habari za mitandao ya kijamii kuekea bajeti ya mwaka wa fedha ya 2024/2025 ili waweze kuandika habari kwa weledi unaotakiwa kuhabarisha umma.
Amesema kuwa wametoa elimu ya miradi ya kimkakati na miradi mbalimbali hivyo waandishi wamepata namna gani ya kuandika habari za wizara ya fedha kulingana na miradi husika katika maeneo husika.
Kingdom amesema kuwa waandishi wa habari za mitandao ya kijamii wanatakiwa kujua namna gani ya kuandika habari za mapato ya ndani ya Halmashauri bila kuchanganya fedha zinazotoka serikali kuu.
“Wananchi na umma wa watanzania kwa ujumla hawawezi kupata habari, Wizara inafanya nini, serikali inatekeleza nini bila ya ninyi na wadau wengine wa vyombo vya habari ambao hawako hapa.” amesema Kingdom