Na. WAF- Dar Es Salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mh. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kufanya utafiti wa ndani ili dawa na chanjo mbalimbali ziweze kuzalishwa nchini huku akiitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuimarisha jambo hilo.
Mhe. Biteko ametoa kauli hiyo leo Mei 14, 2024 Jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 32 wa Wanasayansi ambao umeandaliwa na NIMR.
Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amewahakikishia NIMR pamoja na watafiti wote kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umewekeza vya kutosha kwenye tafiti hasa kwenye sekta ya afya ili kutatua changamoto kama taifa.
“Pamoja na kwamba tunahitaji watu kutoka nje lakini na sisi wenyewe tuwe na uwezo wa kufanya ugunduzi wa ndani. Amesema na kuongeza
“Tumeishaanza utaona kuwa zipo hata dawa zenyewe,chanjo zenyewe lazima tuwe na utafiti ambao utatusaidia pengine zizalishwe hapa ndani kwa manufaa ya watanzania na kutufanya kama Taifa ambalo linakuwa kwa kasi kweli kweli,”amesema Biteko
Aidha, Dkt. Biteko amesema maendeleo mahali popote ili yaweze kutokea lazima kuwe na utafiti ambao umebeba ushahidi wa Kisayansi ili uweze kukupangia wapi unapokwenda na vitu gani utakutana navyo.
Amesema lengo likiwa ni ujiandae mapema na uweze kuwa na matumizi mazuri ya rasilimali.
Hata hivyo ameongeza kuwa maendeleo yoyote yakifanyika kama hakuna utafiti yatakuwa ni maendeleo ya kubahatisha na matokeo yatakayopatikana yatakuwa ni ya kubahatisha.
“Na kutakuwa na kukosea kosea kwingi na matokeo yake rasilimali nyingi zaidi utanitumia.Ndio maana wana Sayansi wanakutana hapa ili kujadili tafiti mbalimbali katika masuala ya afya,”amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molel amesema binadamu wote ni sawa lakini miongoni mwao kuna watu wenye uwezo wa kipekee wenye uwezo wa kuona mambo yasiyoonekana kwa macho ya kawaida.
Amesema tofauti ya Mataifa makubwa yaliyoendelea na Mataifa maskini sio ardhi kubwa ama idadi ya watu ni akili za watu hao.
Amesema Serikali ni namna gani wamewekeza kwa watu hao wenye akili kubwa ambao ndio hao watafiti waliohudhuria Mkutano huo.
Dkt. Mollel amesema kwenye gunduzi za Kisayansi watafiti wanatakiwa kuendelezwa na Serikali ya awamu ya sita inalifanya jambo hilo.
Amesema wanamshukuru Rais kwa kukubali kwamba mojawapo ya kipaumbele katika Wizara ya Afya uwe ni utafiti.
Dkt. Mollel amesema bajeti ijayo watatengeneze mfumo wa kuwatambua wale wenye akili kubwa.
“Si kweli wapo?hata ukikaa pembeni ya mwenzako unakubali kwamba hichi ni kichwa kuliko mimi.Tunataka tufike mahali tuje na Mkakati ni namna gani watu wenye akili watengenezewe mfumo, kwa sababu ifike mahali wasifikirie watoto wao wanaenda shule kwa namna gani,”amesema Dkt. Mollel.
Amesema Rais Samia anahangaika ili uchumi wa Tanzania uweze kukuwa na watafiti waweze kunufaika na tafiti zao.
Hata hivyo Dkt. Mollel amempongeza Mkurugenzi wa NIMR kwa kupeleka watafiti wadogo ndani ya ukumbi huo ambao watajifunza mambo mbalimbali.
“Asanteni kwa kuwalea hawa watoto,asanteni sana, endeleeni kuwalea na kuwafundisha utamaduni wa utafiti Mimi niligoma goma kusoma kwa sababu nilitaka kufundisha shuleni kufikiri nikajikuta nafundishwa kufikirika,”amesema Dkt. Molel.
Amesema kazi waliyonayo watafiti ni kuona namna gani wanatengeneza vitu ambavyo vinatolewa nje ya Tanzania.