Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohammed akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, kuhusiana na kongamano la sita la usafiri wa anga la Jumuiya ya afrika mashariki, kongamano ambalo linatarajiwa Kufanyika mei 15 -16 katika Ukumbi wa Verde Mtoni.
……..
Na Maelezo Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la sita la usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki, linalotarajiwa kufanyika tarehe 15-16 mwezi huu katika Hoteli ya Verde Mtoni.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed amesema zaidi ya wadau 200 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo.
Amesema lengo la Kongamano hilo ni kujadili masuala yanayohusu usalama wa usafiri wa anga na ubunifu wa Teknolojia ambapo nchi wanachama wataweza kuziweka sheria, kanuni na miongozo ya kusimamia masuala ya anga.
Aidha amesema, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki , zitapata fursa za kubadilishana uzoefu na kuweka mipango ya pamoja katika uwekazaji wa miundombinu na huduma bora za anga.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya usimamizi wa anga Tanzania Hamza Johari ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kukubali kuandaa mkutano huo jambo ambalo limeipa heshma kubwa Zanzibar .
Mkurugenzi Johari ambae pia ni Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Taasisi ya udhibiti wa usalama wa usafiri wa anga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CASSOA) amesema Miundombinu ya viwanja vya ndege Zanzibar inakuwa kwa kiasi kikubwa.
Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Taasisi ya Udhibiti na Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CASSOA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo watoa huduma za usafiri wa anga, waendeshaji wa viwanja vya ndege na wadau wengine.
Kauli mbiu katika kongamano hilo ni “Mustakabali wa usafiri wa anga kudumisha mifumo ya usafiri wa anga yenye ustahamilivu, uendelevu, ubunifu na usalama”.