Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala amewataka wadau kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha vitendo vya uvunjifu wa maadili haviendelei ndani ya wilaya hiyo na maeneo yote hatarishi ikiwemo biashara ya ngono pamoja na uharibifu wa mazingira kwa kupiga kelele za mziki mkubwa maeneo yasiyoruhusiwa
Akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa jengo jipya la utawala la halmashauri ya manispaa ya Ilemela kikihusisha wamiliki wa nyumba za kulala wageni, wamiliki wa karakana bubu za magari na wamiliki wa kumbi za starehe Mhe Masala amefafanua kuwa ni jukumu la kila mdau na jamii kwa ujumla kuhakikisha maadili yanalindwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinakoma
“Ningeweza kukaa na wenzangu alaf tukafanya maamuzi ya nyinyi wote kufunga biashara zenu sababu ni sehemu ya kichocheo cha uvunjifu wa maadili maana wengine biashara zenu ndio sehemu za maficho ya dada poa na kaka poa ila tukaona sio busara kuamua bila kuwasikiliza na sisi tunataka tushirikiane tumalize tatizo hili ” alisema
Aidha Mhe Masala amewataka wadau hao kuhakikisha wanalipa kodi za Serikali ikiwemo leseni za biashara, kodi za huduma na za mamlaka ya mapato TRA ili Serikali iweze kutekeleza shughuli za maendeleo pamoja na kukiomba chama cha mapinduzi na jengo la Rock City mall kuongea na wapangaji wake juu ya kufuata masharti ya mikataba ya upangaji maeneo
Kwa upande wake mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Bi Ummy Mohamed Wayayu ameongeza kuwa Serikali haitaacha kumchukulia hatua mtu yeyote anaekwenda kinyume na sheria za nchi na kwamba wadau hao hawataachwa kiholela kama watashindwa kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na mkuu huyo wa wilaya sanjari na kuwataka watendaji wa ngazi za chini kila mmoja kutimiza wajibu wake
Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni ya Antonio inayolalamikiwa kuendesha biashara ya ngono nyakati za usiku mbali na kumshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kufanya nao kikao ameomba kupewa muda ili akashughulikie kero zote zonazolalamikiwa dhidi ya nyumba yake ya kulala wageni huku akiwaasa wafanya biashara wenzake kufata utaratibu huo ili kukomesha biashara ya ngono na vitendo vyengine vya uvunjifu wa maadili
Akihitimisha kikao hicho mkuu wa wilaya ya Ilemela ametoa siku 14 kwa wadau hao kwenda kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa na kwamba baada ya hapo hatua kali za kisheria zitacgukuliwa kwa yeyote atakae kaidi