Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema moduli ya mfumo mpya wa kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki (Complaint and Appeal Management) utaanza kufanya kazi rasmi kuanzia tarehe 1 Julai 2024.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alipokuwa akifanya mahojiano katika kipindi cha Joto la Asubuhi cha Efm Jijini Dar es Salaam kuhusu Moduli mpya ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki.
“Mabadiliko ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, yameweka sharti la lazima kwa taasisi nunuzi na wazabuni kutumia Mfumo wa Kieletroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) ambapo PPAA kwa kushirikiana na PPRA tumejenga moduli mpya ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki ili kukidhi matakwa ya sheria” amesema Bw. Sando
Bw. Sando ameongeza kuwa moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kielektroniki itaanza rasmi tarehe 1 Julai 2024, ambapo pamoja na mambo mengine, amewasihi wazabuni na taasisi nunuzi wa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Pwani kushiriki mfunzo ya awamu ya kwanza kuhusu mfumo huo tarehe 29 na 30 Mei 2024 Jijini Dar es Salaam