Kaimu Mkurugenzi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Regina Mvungi (kulia) akimkabidhi zawadi Mfanyakazi bora wa Mkataba wa muda maalamu 2023/2024 wa TANESCO Wilaya ya Yombo Fundi Umeme Christian Mwaliki katika hafla fupi ya kumpongeza iliyofanyika Mei 10, 2024 jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Regina Mvungi akizungumza jambo katika hafla ya kumpongeza Mfanyakazi bora wa Mkataba wa muda maalamu 2023/2024 wa TANESCO Wilaya ya Yombo Fundi Umeme Christian Mwaliki iliyofanyika Mei 10, 2024 jijini Dar es Salaam.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Yombo Mhandisi Elirehema Makacha akizungumza jambo katika hafla ya kumpongeza Mfanyakazi bora wa Wilaya hiyo.
Picha za matukio mbalimbali
……………..
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Yombo imetoa tuzo kwa mfanyakazi bora anayetekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa wafanyakazi katika shirika wenye mikataba ya kudumu pamoja na wale wa muda maalum.
Akizungumza Mei 10, 2024 katika hafla ya kumpongeza mfanyakazi bora wa muda maalum iliyofanyika katika ofisi za TANESCO Wilaya Yombo iliyopo Kata ya Vituka jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Regina Mvungi, amewapongeza wafanyakazi wa TANESCO Wilaya ya Yombo kwa kuendelea kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano.
Mhandisi Mvungi amesema kuwa wakati umefika kwa wafanyakazi wa Mikoa na Wilaya kuiga mazuri ambayo wanafanya Wilaya ya Yombo ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa kutoa huduma bora kwa wateja.
“Wafanyakazi wa Wilaya ya Yombo wana upendo ambao sijawai kuona sehemu nyengine, ni muhimu watumishi wengine kuiga mfano huu mzuri wa kuendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora” amesema Mhandisi Mvungi.
Aliongezea kwa kusema, Mkurugenzi wa kanda ya mashariki amemuagiza kuja kuungana na wafanyakazi wa Wilaya ya Yombo na kumkabidhi kitita cha shilingi laki nne pamoja na kumpatia safari ya kwenda kujifunza maeneo mengine ndani ya Shirika.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola amesisitiza umuhimu wa watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu na maadili jambo ambalo ni rafiki katika kuleta matokeo chanya katika shirika.
Aidha, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Yombo Mhandisi Elirehema Makacha, amesema kuwa wafanyakazi wote wanatekeleza majukumu yao vizuri ila ubunifu unaofanywa na baadhi yao katika utendaji wameoneka kuwa bora zaidi kuliko wengine.
Mhandisi Makacha alieleza kuwa kazi yenye ubunifu, uweledi na maadili ni vitu ambayo vinamtofautisha mtu mmoja na mwengine, hivyo kuwatambua wafanyakazi wa aina hiyo ni muhimu kutokana inaleta hamasa katika utendaji wenye kuleta tija. “Kutambua juhudi za mfanyakazi ni kuongeza hamasa kwa wengine ili waongeze ubunifu katika uekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kufikia kiwango cha kuitwa mfanyakazi bora” amesema Mhandisi Makacha.
Nae mfanyakazi bora wa Mkataba wa muda maalamu 2023/2024 Christian Mwaliki (fundi) amewashuru wafanyakazi wezake na uongozi kwa kumtambua kuwa mfanyakazi bora kwa kupendekeza jina lake, huku akieleza kuwa juhudi pamoja na kuzingatia maadili katika utendaji wa kazi ni siri ya mafanikio yake.
Halfa hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Diwani Kata ya Sandali, Mhe. Christopher, Viongozi wa serikali za mitaa, wateja wakubwa wa Wilaya ya Yombo pamoja na menejimenti ya Mkoa wa Temeke.