TAASISI ya Binti Lindi Initiative imegawa mizinga 50 ya kufugia nyuki kwa vikundi vitano ya Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi vyenye watu zaidi ya 50.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mizinga hiyo 50 ya kufugia nyuki, mkurungenzi wa taasisi ya Binti Lindi initiative Kijakazi Yunus alisema kuwa amekabidhi mizinga hiyo kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi wa wilaya ya Nachingwea na Lindi kwa ujumla.
Yunus alisema kuwa anaunga mkono juhudi za Rais Dr Samia Suluhu Hassan katika kuhifadhi mazingira na kukuza uchumi wa wananchi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Aidha Yunus alisema kwamba taasisi hiyo inajihusisha kusaidia mabinti na wanawake kwenye sekta ya elimu na uchumi kwa sababu kumekuwa na mmong’onyoko wa maadili unaopelekea kutokea mimba nyingi za utotoni ambazo mara nyingi kukatisha ndoto za mabinti wengi.
Yunus alisema kwamba wanawake wakiwa na uchumi mzuri unasaidia maendeleo ya taifa lakini kwa sasa maadili ya watanzania yameporomoka kwa kiasi kikubwa hivyo taasisi ya Binti Lindi initiative inatoa elimu ya umuhimu wa kuwa na maadili mazuri.
Kwa upande wake afisa tarafa ya Nambambo Christopher Mkuchika alimpongeza mkurugenzi wa taasisi ya Binti Lindi initiative Kijakazi Yunus kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kutoa elimu ya malezi na uchumi kwa mabinti na wanawake.