Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga Bi. Pili Mnyema ameipongeza timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na DKt. Rashid Mfaume kwa kufanya ziara iliyobaini mapungufu na kutoa maelekezo ya kuboresha utoaji wa huduma za Afya katika mkoa wa Tanga.
Bi. Mnyema ametoa pongezi hizo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya usimamizi shirikishi kilicho kutanisha timu ya Afya,Ustawi wa jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na timu za uendeshaji wa huduma za Afya za Halmashauri (CHMTs) na mkoa (RHMT) kilichofanyika katika ofisi ya mkuu wa mkoa.
Katika kikao hicho Mnyema amekiri kupokea ushauri na maelekezo yaliyotolewa na timu hiyo na kuahidi kutekeleza ifikapo Juni 30,2024 huku akiwataka waganga wakuu wa Halmashauri za Korogwe Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwenda kushughulikia mapungufu yaliyobainishwa katika maeneo ya kutolea huduma za Afya.
“Tunakwenda lakini mnatukumbusha tuongeze kasi lakini kwenye yale ya kawaida hayatakiwi kuwepo mfano milango ya wodi inatakiwa iweje,sinki linatakiwa liweje kwasababu haiingii akilini mkurugenzi atoke wizarani aje pale kwenye kituo cha Afya na DMO unaenda pale kutuoni na husemi” amesema Pili Mnyema RAS Tanga
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amezikumbusha timu za uendeshaji wa Huduma za Afya za Halmashauri (CHMT) na Mikoa (RHMT) kufanya ziara shirikishi katika maeneo ya kutolea huduma za Afya.
Timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ikiongozwa na mkurugenzi DKt. Rashid Mfaume imeelekea mkoa wa Kilimanjaro kwaajili ya ziara ya usimamizi shirikishi na ukaguzi wa miradi ya kutolea huduma za Afya katika mkoani humo.