Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
Mei 11
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani ,Mwinshehe Mlao
amewaagiza madiwani mkoani humo kuwa na maadili , kuacha kutumia mitandao ya kijamii vibaya pamoja na kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 .
Aidha amewasisitiza madiwani pamoja na wanaCCM kuacha mara moja kujichukulia dhamana ya kuwa wasemaji katika mitandao ama vijiwe bila kuwa na uhalali huo.
Mlao alitoa maagizo hayo ,wakati alipokutana na madiwani wa Halmashauri zote za Mkoa huo katika kikao cha tathmini kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, kikao kilichofanyika Wilayani Mkuranga.
” Mtu yeyote atakayekiuka maadili ya chama chetu kwa kutukana mitandaoni, ninaagiza kuanzia sasa aitwe katika vikao husika na kujadiliwa sambamba na kuchukuliwa hatua za kinidhamu”* alisema Mlao.
Mlao, aliwakumbusha madiwani hao kuwa na maadili, kuepuka udini, na wajenge tabia ya kuwa karibu na wananchi kwa kufanya ziara za kusikiliza na kutatua kero katika maeneo yao.
Aliwaasa kuendelea kushirikiana na wanachama kusemea utekelezaji wa ilani na makubwa yanayofanywa na Serikali.
Nae Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani ,Bernard Ghaty aliwatahadharisha madiwani kuhakikisha hawapotezi Mitaa,Viijiji wala Vitongoji katika kata zao.
“Lengo la Chama Chetu ni kuhakikisha Mitaa, Vijiji na Vitongoji vyote vinarudi CCM, na mkumbuke Mwenyekiti wetu alipokea kijiti hicho nafasi zote zikiwa zipo CCM na ndoto yake ni kuona vijiti vyote vinarudi CCM” alifafanua Ghaty.
Aliwasihi madiwani wa viti maalum kufanya ziara katika Halmashauri zao na si kufanya katika kata wanazoishi pekee badala yake waende wakakiimarishe Chama na kushughulika na maswala yote ya kuisimamia Halmashauri kwa mujibu wa Sheria na kanuni katika majukumu yao.
Madiwani hao wameahidi kwenda kutekeleza maagizo yaliyotolewa katika kikao hicho na watafanya kazi kwa bidii na uzalendo ili kuendelea kumuunga mkono, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan.
Aliwataka madiwani wanaotokana na CCM kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 kwa kuhakikisha wanatatua changamoto za wananchi ili CCM kishinde kwa kishindo.