Na Mwandishi Wetu, Kilosa
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, amesema kijana, Lazaro Ndutu, amefariki dunia baada ya kupigwa mapanga sehemu za kichwani ndani ya hifadhi ya msitu wa kijiji cha Kigunga katika kitongoji cha Kikuyu Tarafa ya Ulaya, kata ya Zombo.
Shaka ameyasema hayo leo wakati akitoa ufafanuzi wa tukio hilo kwa vyombo vya habari ambapo amesema mtuhumiwa alipata majeraha hayo jana majira saa mbili asubuhi na kijana huyo alifariki usiku wa kuamkia leo.
“Ugomvi wa kuvamia eneo kila mmoja alisema ni lake huko msituni walipovamia na kujeruhiwa kwa Ndutu vijana hao wametokea Mkoani Tabora na kuja kuvamia msitu amesema Shaka.
Aidha, Shaka amesema mapema Machi mwaka huu alipokea taarifa za wananchi kuvamia msitu huo na serikali ilichukua hatua za kupiga marufu uvamizi huo na kuweka doria ili kudhibiti vitendo hivyo.
“Ni kweli vyombo vya ulinzi na usalama vinamshikilia kijana Dotto Lusuka (21) kwa tuhuma za kuhusika na mauji hayo ambapo kijana mwingine Suma Lusaka mdogo wake na mtuhumiwa aliyekamatwa anatafutwa na jeshi la polisi baada ya kutoroka lilipotokea tukio” amesema Shaka na kuongeza kuwa;
“Tulipiga marufu na kuimarisha doria katika hifadhi za misituni baada kupata taarifa za uvamizi na kuelekeza kwa jeshi la polisi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Halmashauri kusimamia matumizi na kulinda hifadhi za misitu na juhudi kadhaa kuchukuliwa lakini wananchi wamekuwa wakivamia kwa siri na kushtukiza wakati mwingine kutaka kujichukulia sheria mkononi, kukata miti, kuchoma mkaa na kufanya uharibifu wa mazingira,”.
Alibainisha kuwa mipango ya serikali ni kuhakikisha kuwa hifadhi za misitu na rasimali zote muhimu wilayani humo zinaendelea kuwekewa mikakati madhubuti ili kunusuru athari zaidi za kimazingira na maafa makubwa kuweza kutokea
“Serikali inalaani vikali mauaji haya ambayo kimsingi ni kinyume na utu na ubinadamu, kitendo cha kumkata kata binadamu mwenzio kama nyama ni ukatili uliopotiliza na halitafumbiwa macho na kwa sasa tunaviachia vyombo vya Ulinzi na Usalama viendele na hatua za kisheria,” alisema.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya huyo alionya tabia ya wananchi kujichukukia sheria mkononi kwa kuwa kufanya husbabisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo na kwamba serikali itamchukulia hatua kila atakayebainika kuhusika.
Aliwasihi wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya Dola na serikali ya kijiji kila wanapobaini tatizo lolote ili lishughulikiwe katika njia zilizo sahihi na kwa wakati.