Na Takdir Ali. Maelezo.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban ameliagiza Baraza la ushindani halali wa Biashara Zanzibar (ZFCT) kushuka chini kwa wananchi ili waweze kulifahamu na kuweza kulitumia kama linavyotakiwa.
Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Zura Maisara wakati alipokuwa akizinduwa Baraza la pili la Usindani halali wa biashara Biashara Zanzibar.
Amesema Baraza hilo bado halijawafikia na kutambulika kwa Wananchi ipasavyo hivyo amewataka kuweka mikakati Madhubuti ya kutoa elimu ili kuwafikia wananchi wengi wa Mjini na Vijijini.
“Ni lazima Baraza letu lishuke chini kwa Wadau, walielewe na wajuwe sehemu ya kupeleka malalamiko yao wakati yanapotokezea ili kuweza kupata haki zao na sio kukimbilia Mahakamani na kwa Viongozi.” Alisema Waziri Shaaban.
Amefahamisha kuwa, kuna baadhi ya Mamlaka za biashara zinatoa maamuzi yasio mazuri na wanaofanya vitendo hivyo hawajafika katika Baraza kupeleka malalamiko yao jambo ambalo linaonyesha kuwa bado uelewa ni mdogo kwa jamii.
Aidha amewapongeza Wajumbe walioteuliwa na kusema anaamini watatoa mchango mkubwa katika kuliendesha baraza hilo ili liweze kufikia malengo yaliopangwa na Serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani halali wa Biashara Gorge Joseph Kazi amesema lengo la Baraza hilo ni kulinda mwenendo nzima wa biashara na kuzuia mienendo ya biashara isio ya ushindani,bidhaa bandia, matumizi mabaya ya nguvu za soko.
Aidha amesema lengo jengine ni muingano ya makampuni na makubaliano yasio ya ushindani kwa kuzingatia maslahi na ustawi wa mtumiaji wa bidhaa na huduma bila ya kuathiri ukuwaji wa Uchumi wa Soko.
Mbali na hayo amewataka Wajumbe walioteuliwa kutekeleza majukumu waliopangiwa kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kulisaidii baraza kuweza kufikia malengo na dhamira mahsusi ya kuanzishwa kwake na kuweza kuleta manufaa kwa wadau wote wa biashara,wananchi na kunyanyua Uchumi wa Taifa letu.
Kwa uapande wake Naibu katibu mkuu wa Wizara ya biashara na maendeleo ya viwanda Zanzibar Said Seif Mzee ameahidi kuwa wizara itatoa ushirikiano wa kutosha na kuwaomba kupeleka malalamiko yao pananpotokea tatizo lolote ili waweze kukaa pamoja na kulitafutia ufumbuzi unaofaa.
Nao baadhi ya watendaji wa Baraza la Ushindani halali wa biashara wakiongozwa na Kaimu Mrajisi wa Baraza hilo Thneyuu Mabrouk Hassan wameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliotolewa na kuwaomba Viongozi, Wadau na Wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kuliendesha baraza hilo na kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.