Taarifa iliyotufikia kutoka Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika inasema Mei 09, 2024 mbele ya Mhe. Sydney Nindi, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo imefunguliwa kesi ya Jinai namba CC. 12307/2024 ya Jamhuri inayowakabili Bw. PIUS EMMANUEL LYAMBISE na NESTORI FRANSISKO GABULIELI (Mgambo wa Kijiji cha Majalila, Kata ya Majalila, Wilaya ya Tanganyika, Mkoani Katavi.)
PIUS LYAMBISE na NESTORI GABULIELI wanashtakiwa kwa tuhuma za kosa la kuomba hongo ya Sh. 200,000/- kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2022.
Akisoma hati ya Mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Amos Mwalwanda amesema, washtakiwa hao mnamo tarehe 25 Aprili, 2024 waliomba hongo hiyo kutoka kwa DEVIDI ELIAS SHEM na ALPHANS JAPHET BWANGARO wa Kijiji cha Kazima, Kata ya Kazima, Wilaya ya Mpanda ili wawaachie baada ya kuwakamata wakisafirisha mbao kutoka Tanganyika kwenda Mpanda bila kibali kinyume na utaratibu.
Washtakiwa wamekana kosa na wamepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana.