Kaimu Naibu Rasi Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba akizungumza jambo wakati akifungua mafunzo ya usalama wa kimtandao (Cyber Security) kwa watumishi wa chuo hicho yaliofanyika leo Mei 9, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama wa kimtandao (Cyber Security) Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kitengo cha Sayansi na Teknolojia, Idara ya Sayansi za Kompyuta Dkt. Morice Daudi akizungumza jambo wakati akiwafundisha watumishi wa chuo hicho.
Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wakiwa kaika mafunzo ya kujengewa uwezo kuhusu usalama wa kimtandao (Cyber Security)
Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja.
……….
Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam wamepewa mafunzo ya usalama wa kimtandao (Cyber Security) kwa ajili ya kuwasaidia kujilinda na uhalifu wa kimtandano katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, jambo ambalo litasaidia kuwa uelewa mkubwa wa kuepuka madhara kabla ya kuwategemea idara za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza leo Mei 9, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya usalama wa kimtandao (Cyber Security), Kaimu Naibu Rasi Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba, amesema kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa sababu kwa sasa asilimia kubwa ya watumishi wanatumia mitandao katika utekelezaji wa majukumu.
Dkt. Komba amesema kuwa ni vizuri watumishi kujua namna ya kujikinga na waharifu wa kimtandao ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza.
“Mtandao unatusaidia kufanya kazi vizuri, lakini ni muhimu kujua namna ya kujilinda wakati unatumia ili kutojiingiza katika matatizo na kujikuta unaharibu mambo mengine katika utekelezaji wa majukumu. ” Alisema Dkt. Komba.
Aidha, Dkt. Komba ameongeza kuwa teknolojia inakua kila siku; hivyo, watumishi wanapaswa kupewa mafunzo daima ili kuongeza ufanisi katika matumizi ya mitandao.
Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kitengo cha Sayansi na Teknolojia, Idara ya Sayansi za Kompyuta Dkt. Morice Daudi, amesema kuwa lengo la mafunzo ni kutoa elimu kwa watumishi kuhusu usalama mitandao na namna ya kujikinga.
Dkt. Daudi amesema kuwa mafunzo hayo yatakisaidia Chuo katika kuhakikisha mifumo yake yote inayotumia mifumo ya kompyuta kuwa salama na kuleta tija kwa Chuo na taifa kwa ujumla.
“Sehemu kubwa ya uharifu wa kimtandao inatokana na tabia za watumiaji. Mifumo ya kompyuta ina ulinzi wake kupitia programu mbalimbali; hivyo, ni vizuri watumishi kupata elimu hasa maeneo ambayo yanashambuliwa zaidi ili wajikinge”. Amesema Dkt. Daudi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Chuo Kikuu Mzumbe wa kuhakikisha watumishi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe (Kampasi Kuu Morogoro, Ndaki ya Mbeya, na Ndaki Dar es Salaam) wanapata elimu sahihi ya jinsi ya kujikinga na uhalifu wa mtandao wanapotekeleza majukumu yao