WITO umetolewa kwa Watanzania na Wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi,kutembelea na kuwekeza katika hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo kanda ya kusini magharibi mwa Tanzania kwa lengo la kujionea na kujifunza mambo mbalimbali yanayopatikana katika hifadhi hiyo.
Miongoni mwa utalii unaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na wingi wa Viboko katika mito na maziwa yaliyopo katika hifadhi hiyo ambao wanabeba nembo ya hifadhi,Wanyamapori wakiwemo Tembo, Twiga,Pundamilia,Swala,Nyati,Simba,Ndege aina mbalimbai pamoja na wanyama wengine.
Wito huo umetolewa mkoani Katavi na Mhifadhi Mwandamizi ambaye pia ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Hifadhi hiyo ya Taifa ya Katavi,Manendo Maziku wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya hali ya utalii katika hifadhi hiyo.
Maziku alisema mtu atakapo tembelea hifadhi hiyo atapata fursa ya kupumzika na kujifunza mambo mbalimbali ambapo katika hifadhi nyingine hayapo.
”Mfano unapoingia katika lango la hifadhi yetu ya Katavi kuna Mto Katuma ambao unabeba Viboko wengi na Mamba na hiyo inakuwa ni ishara kuwa umeingia katika hifadhi yetu ya Katavi hivyo inakupa fursa ya kujua namna ya Viboko na Mamba wanavyoishi katika mto huo,”alisema na kuongeza
”Nitoe rai kwa watanzania wenzangu kujenga tabia za kutembelea hifadhi zetu kwani hazijawekwa kwa watu fulani bali zipo kwaajili ya wote,tunapaswa kutembelea kutumia muda wa mapumziko katika kutembelea hifadhi zetu,”alisema.
Aidha alisema hifadhi ya Katavi ni moja ya hifadhi kongwe nchini ambayo ilianza mwaka 1974 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 2253,lakini baada ya ikolojia kuzidi kukuwa hifadhi hiyo imeongezeka ukubwa na kufikia Kilomita za mraba 4471 tangu mwaka 1997.
Maziku alisema hifadhi hiyo inafikika kwa njia mbalimbali ikiwemo Reli,Barabara pamoja na njia ya anga(Ndege)ambapo kuna uwanja uliopo ndani ya hifadhi kwaajili ya watalii na mwingine upo Katavi mjini ambao unatumiwa na watu mbalimbali.
Akizungumzia suala la Miundombinu ndani ya hifadhi,Maziku alisema kutokana na mvua za masika kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi,ikiwemo mkoani humo ambapo zimeweza kuharibu baadhi ya miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi pamoja na vivuko kukatika.
”Ndani ya hifadhi zetu miundombinu yetu imeharibika ikiwemo barabara kujaa maji na vivuko kukatika,ila juhudi zimeanza kufanyika katika hifadhi yetu ambapo tayari tumehainisha barabara zote zilizoharibika na kushindwa kuingilika katika hifadhi kwaajili ya kuanza kutengeneza kwaajili ya msimu wa utalii unaokuja,”alisema.
Kwa Upande wake Mhifadhi Mwandamizi ambaye pia Mhifadhi wa Utalii wa hifadhi hiyo ya Katavi, Anthony Shirima alisema hifadhi hiyo ni ya tano kwa ukubwa baada ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Ruaha,Seregeti, na Burugi Chato.
Alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna uoto wa asili ambapo kuna uwanda wa nyasi,maziwa ya msimu ya Chada na Katavi,mabwawa na uondo kando ya mito.
Alisema hifadhi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa miundombinu ndani ya hifadhi hususan kipindi hiki ambacho cha mvua za msimu kinafanya wanyama kutoonekana vizuri.
”Maji yamejaa kila mahali hadi katika barabara za hifadhini inafanya wanyama kutoonekana vizuri hasa viboko kwani wanakuwa wanaenda pembezoni mwa mito kwaajili ya kupata hewa,kutokana na kuzidiwa kwa maji mengi”alisema