Na Mwandishi wetu,Katavi
WANANCHI waishio vijiji vya pembezoni mwa hifadhi ya Taifa Katavi waishukuru hifadhi hiyo kwa kuendelea kuwasaidia katika kuwaletea maendeleo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa bweni,Madarasa ,Vituo vya Afya,Utoaji wa mizinga kwa wanawake pamoja na uchimbaji wa kisima cha maji.
Akizungumza waandishi wa habari jana,walisema hifadhi hiyo imekuwa mstari wa mbele kwao katika kuhakikisha inawasaidia wananchi waishio katika vijiji hivyo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Siwajibu Wemba Kaimu Mtendaji Kijiji cha Stalike Mkoani Katavi amesema uwepo wa hifadhi hiyo umeweza kuwaletea maendeleo mbalimbali ambayo yamekuwa msaada kwao kwani miaka ya nyuma hawakuwa nayo.
Amesema hifadhi hiyo imekuwa ikiwasaidia katika kuhakikisha vijiji vyao vinapata maendeleo na kwa kuwajengea miundombinu mbalimbali ambayo imewasaidia katika kuhakikisha wanakuwa na afya nzuri,watoto wao wanauhakika wa kupata elimu pamoja na kuwainua wanawake kiuchumi katika kuwapatia mizinga.
”Kwa kweli tunaushirikiano mzuri sana na Ofisi ya hifadhi ya taifa ya Katavi kwa kutusaidia vitu mbalimbali na endapo kama kuna changamoto yoyote tunawafata na kuzungumza nao na hawasiti kutusaidia,”amesema Wemba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji Jirani cha Igongo ,Emphraimu Wamburu ameipongeza na kuishukuru hifadhi hiyo kwa kuwatendea vitu vingi katika vijiji vyao bila ubaguzi wowote.
Amesema pamoja na mambo mengine wameweza kuchimbiwa visima ambapo awali vilikuwepo ila vilikuwa vichache,hivyo wamekuwa wanafurahia ushirikiano huo kwao.
Amesema mbali na kuipongeza hifadhi hiyo pia ametaja baadhi ya changamoto ambayo wanakabiliana nayo ikiwemo wanyama kufanya uharibifu katika mashamba yao wakiwemo wanyama aina ya tembo na kiboko kuvuka katika hifadhi na kuja katika maeneo ya vijiji na kuharibu mazao yao.
”Tunashukuru watu wa hifadhi hii wamekuwa wanakuja kutusaidia na kuwarudisha wanyama ila wanapokuwa katika doria zao askari upungua hivyo uharibifu kuwa mkubwa kutokana na kushindwa kuwarudisha wanyama hao hifadhini,”amesema na kuongeza
”Ukiangalia hali kama hii bado kikwazo kikubwa kwao licha ya kifuta machozi tunachopewa hakitoshi,hivyo tunaiomba Serikali na Shirika kutupigania huko mbele walau kifuta machozi kiongezeke na jitihada kubwa ya kurejesha wanyama katika hifadhi iongezeke na iwe kubwa,”amesema.
Amesema hifadhi hizi zinakuwa na manufaa makubwa kwa watanzania wote na sio vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo pekee kwa kuwaletea maendeleo katika taifa.
Kwa Upande wake Afisa Uhifadhi daraja la pili ambaye pia ni Kaimu Mhifadhi wa Idara ya Mahusiano ya Jamii,Meleji Mollel amesema hifadhi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mahusiano mazuri na vijiji kwa kuwasogezea huduma mbalimbali.
Amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa shule za msingi,sekondari na jamii kuhusu madhara ya kulima karibu na hifadhi hiyo pamoja na namna ya wananchi hao kuishi na wanyama hao pamoja na kukabiliana na wanyama waharibifu .
”Wanyama pori hawana akili kama binadamu na hawana utashi wa kuangalia mipaka kwamba sasa wanatoka nje ya hifadhi au sasa wanaingia katika mashamba ya binadamu,hivyo ni muhimu wananchi kuwapa elimu ili kukabiliana nao,”amesema na kuongeza.
”Kitengo cha jamii ni kuwapa elimu kwa namna ya kukabiliana na wanyama hao na endapo wanapowaona wanaingia katika vijiji vyao uwa tunawaambia watoe taarifa sahihi ili vikosi vichukue hatua ya kuwarudisha wanyama hifadhini bila kuleta madhara katika makazi yao,”amesema.
Aidha amesema tayari wamejenga bweni katika Shule ya Sekondari ya Sitalike,Ujenzi wa Darasa katika shule ya msingi Sitalike,Ujenzi wa vituo vya afya katika kijiji ca Sitalike na Mwamapuli,Kuwachimbia kisima katika kijiji cha Luchima pamoja na kuwapatia mizinga 100 kwaajili ya vikundi vya wanawake wa kijiji cha Sitalike na Kibaoni.
Amesema mbali na elimu ya kukabiliana na wanyama waharibifu pia wamekuwa wakiwapatia elimu ya uhifadhi wa mazingira,Utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kutunza wanyamapori ili vizazi vijavyo waweze kuviona.
Akizungumzia namna ya kutatua changamoto za wanyamapori kuingia vijijini,Mollel amesema wakipokea taarifa uwa wanafika eneo la tukio na kuwarudisha wanyama hao hifadhini,kuwasiliana na mamlaka nyingine ikiwemo Tawa au Halmashauri kama kuna mazao ya binadamu yameharibiwa kuweza kuweza kuangalia taratibu mbalimbali za fidia.
”Tumekuwa tunashirikiana na kuhakikisha wanyamapori wanapoingia katika vijiji hawawadhuru binadamu wala mazao yao hasa hifadhi ikishapata taarifa,”amesema.