Wizara, Taasisi, Mamlaka, wadau na sekta binafsi zimeagizwa kuzingatia matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kulinda mazingira na athari nyingine zinazotokana na nishati isiyo safi.
Agizo hilo limetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo (Mei 8, 2024) Jijini Dar es salaam wakati akizindua Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia 2024 – 2034.
“Wizara ya Nishati ihakikishe inafikisha Mkakati huu kwa wadau wote muhimu kwa kutumia njia rasmi, Mkakati uwe kwa lugha zote za kingereza na kiswahili na uwekwe katika mitandao ili kusaidia wananchi waweze kuipata kwa urahisi, mkutane na sekta zingine na kubaini maeneo ya kufanyia kazi ili kuweka bei himilivu kwa wananchi ili waweze kutumia Nishati Safi ya Kupikia”, amesema Rais Samia.
Maelekezo mengine ni “Mkakati uonekane kwenye Dira ya Taifa ya mwaka 2050, TAMISEMI iboreshe mikataba kati yake na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Mikoa wafanye hivyo kwa Wakuu wa Wilaya ili kuhimiza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia”, amesisitiza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameitaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuendelea kutekeleza jukumu lake la kusambaza nishati vijijini ikiwemo Nishati Safi ya Kupikia.
Pia, ameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa na kutoa katazo la matumizi ya nishati isiyo safi kwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya watu 100. Ameelekeza taarifa rasmi kuhusu utekelezaji huo iwasilishwe ifikapo Agosti, 2024.
Aidha, Rais Samia amesema kuwa mkakati huo wa kitaifa pia utachangia jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kutokana na uharibifu wa misitu ambao huchangiwa na shughuli za kibinadamu ambapo inakadiriwa kuwa hekta 469,000 za misitu hupotea kutokana na matumizi ya mkaa na kuni.
Naye, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuimarisha upatikanaji wa malighafi na raslimali za nishati hiyo.
“Mkakati huu ambao upo chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu utatakelezwa kwa gharama ya shilingi trilioni 4.6 umezingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa”, amesema Mhe. Majaliwa
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yatasaidia wanawake na vijana kupata muda mwingi wa kufanya kazi sambamba na kulinda afya zao.
“Mhe. Rais tunakushukuru sana kwa programu hii ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo itasaidia kupunguza athari kwa wanawake na vijana kwa kutumia muda mwingi kutafuta kuni na hata kupata magonjwa yanayosababishwa na moshi’’, amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Katika kutekeleza agizo lako la kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia tutahakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia Nishati Safi ya Kupikia”.