Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Mhe. Dorothy George Kilave na Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Cosato David Chumi, kuhusu mpango wa Serikali wa kuwasaidia wafanyabiashara kulipwa madai yao pamoja na riba wanapo cheleweshewa malipo na pia Serikali itaanza lini kurejesha asilimia 20 (Retention) ya Kodi ya Ardhi kwenye Halmashauri. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)
……..
Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa ulipaji wa madai yanayotokana na kupokelewa kwa bidhaa au huduma huzingatia masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi iliyoingiwa kati ya Serikali na mtoa huduma.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba(Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Temeke Mhe. Dorothy George Kilave, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwasaidia wafanyabiashara kulipwa madai na riba wanapo cheleweshewa malipo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali hulipa au hulipwa riba iwapo masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi imekiukwa.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyo la kuitaka Serikali kutoa maelekezo ili wazabuni walipwe madai yao pamoja na riba wakicheleweshewa fedha baada ya kuingia mikataba, Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inaangalia namna ya kuliweka jambo hilo kwenye kanuni za ununuzi ili kuwalinda wazabuni wa ndani ambao si tu kwamba wanacheleweshewa malipo yao, bali pia Wakandarasi kutoka nje wanaoingia nao mikataba ya kazi huwalipa kwa shilingi ya Tanzania wakati wao wanalipwa kwa dola za Marekani.
Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali inakamilisha kanunui za ununuzi baada ya Bunge kurekebisha Sheria ya ununuzi wa umma, lengo ni kuhakikisha wakandarasi wa ndani wananufaika na kazi wanazozifanya.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Cosato David Chumi, kuhusu muda ambao Serikali itaanza kurejesha asilimia 20 (Retention) ya Kodi ya Ardhi kwenye Halmashauri kama ilivyopitishwa katika Sheria ya Fedha 2023/2024, Dkt. Nchemba alisema kuwa urejeshwaji wa kodi hiyo utaanza baada ya zoezi la kukusanya kodi ya ardhi litakapoanza kutekelezwa rasmi na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Utaratibu wa kurejesha asilimia 20 ya kodi ya ardhi kwenye Halmashauri unatarajiwa kuanza kabla au ifikapo Juni 30, 2024”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa hadi Aprili 2024, taratibu za kuwezesha halmashauri kuanza kukusanya kodi ya ardhi hazikukamilika hususan kufungamanisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na mfumo wa kukusanya mapato ya halmashauri – TAUSI.
Alisema mwaka 2023/24, Serikali ilifanya maboresho ya ukusanyaji wa kodi ya ardhi ambapo halmashauri kupitia Ofisi ya Rais -TAMISEMI zinatakiwa kukusanya kodi ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.