Mkuu wa wilaya ya Iringa Komred Kheri James amefungua kikao kazi cha watunza kumbukumbu na nyaraka Tanzania, kilichofanyika kitaifa wilayani Iringa na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa yote nchini.
Akizungumza katika kikao hicho Komred Kheri James ameeleza kuwa Serikali inatambua na kuthamini sana mchango wa tasnia ya menejimenti ya kumbukumbu katika kuharakisha na kusaidia kufanya maamuzi na sahihi kwa haki na ustawi.
Aidha Komred Kheri James ameeleza kuwa Serikali kupitia ofisi ya Katibu Mkuu utumishi imeendelea kutoa maelekezo na miongozo ya namna bora ya utunzaji wa nyaraka.
Pamoja na mambo mengine Komred Kheri James amesisitiza umuhimu wa wanataaluma hao kuwa waadilifu na kuzingatia maadili ya kazi.
Akitoa Shukran kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Mwenyekiti wa TRAMPA Bi. Devotha Mrope amewashukuru sana waajiri na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuilea na kuisimamia vyema kada hiyo muhimu katika utumishi, na hivyo ameeahidi kutumia kikao hicho kukumbushana misingi na wajibu ili kuongeza tija katika utendaji.
Kikao kazi hiki maalumu kinatarajia kufanyika kwa siku tatu na kukamilika siku ya Alhamisi ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora Mh.George Simbachawene anatarajia kuhutubia na kuhairisha kikao hicho cha mafunzo.