Afisa Maendeleo Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Christabela Ngowi akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Tukuyu wilayani Rungwe wakati wizara hiyo ilipoendesha kampeni maalumu dhidi ya Usalama wa Watoto Mitandaoni.(Picha na Joachim Nyambo)
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya wakimsikiliza Afisa Maendeleo Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Christabela Ngowi wakati wizara hiyo ilipoendesha kampeni maalumu dhidi ya Usalama wa Watoto Mitandaoni.(Picha na Joachim Nyambo)
……………………
Na Joachim Nyambo, Rungwe.
JAMII inaaswa kuwakinga watoto dhidi ya mitandao ya kijamii iliyo na maudhui hususani picha au vielelezo vinavyokinzana na Mila na desturi pamoja na Sheria za nchi.
Afisa Maendeleo Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Christabela Ngowi amesisitiza hayo wilayani hapa wakati wizara hiyo ilipoendesha kampeni maalumu dhidi ya Usalama wa Watoto Mitandaoni.
Wizara imeendesha kampeni hiyo katika shule ya Msingi Tukuyu ikiwa miongoni mwa shule tisa zaidi zitakazofikiwa lengo mahususi likiwa ni kuwajengea ustawi bora watoto na kuwaepusha na vihatarishi vinavyoweza kurudisha nyuma makuzi stahiki na malezi katika jamii.
Ngowi amesema bado jamii inapaswa kuwajibika katika kuwalinda watoto dhidi ya maudhui potofu yaliyopo kwenye mitandao ya kijamii kwakuwa haiwajengi bali inabomoa kizazi cha sasa na kijacho kwa kuharibu makuzi.
Ametaja baadhi ya maudhui yasiyofaa mtandaoni kuwa ni pamoja na picha za ngono, matumizi ya madawa ya kulevya, ukatili wa aina mbalimbali , udhalilishaji na vitisho kwa kutumia picha, sambamba na yenye nie ye kumrubuni mtoto mtandaoni.
Afisa huyo amesema iwapo jamii itapuuza maudhui hayo ni kuwaacha watoto kuendelea kukutana nayo mitandaoni ni wazi mitandao ya kijamii itatumika kutimiza malengo ya watu wachache wanaotaka kuharibu maadili ndani ya jamii.
Ameipongeza serikali nchini kwa kuendelea kutoa miongozo ya utoaji wa maudhui Mtandaoni akisema kufanya hivyo kutasaidia kuboresha ustawi wa watoto na jamii yote kwa ujumla.
Watoto walio na umri wa chini ya miaka nane wanaotajwa kwenye Programu Jumuishi ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) wanatajwa kuwa katika hatari zaidi ya kuathiriwa na maudhui ya mitandaoni iwapo hawatosimamiwa kutokana na kundi lao kuwa kwenye eneo muhimu la ukuaji hasa upande wa ubongo.
Muhimu kwa jamii ni kuwa makini juu ya mitandao ya kijamii inayofuatiliwa na watoto kwa kujiridhisha juu ya maudhui yake kabla ya kuwaruhusu kuitembelea ili iwapo watabaini kuwepo kwa mapungufu wasiruhusu kuifikia.
Tayari serikali ilikwishachukua taratibu mbalimbali za udhibiti wa maudhui mitandaoni ambapo Kanuni za maudhui mtandaoni za Mwaka 2022 zilitengenezwa chini ya Sheria ya Mawasiliano na Posta ya Mwaka 2010(Epoca) ambapo malengo ya kanuni hizo ni kusimamia na kuendesha maudhui yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari vya kimtandao.
Kanuni hizi pia zinatoa utaratibu wa namna ya usajirli wa watoa huduma za watumiaji wa maudhui mtandaoni vikiwemo vyombo vya habari mtandaoni kama redio na televisheni na mitandao ya kijamii kama blogs, facebook, whatsapp, na instagram.
Wakili wa kujitegemea James Marenga anasema kanuni za mtandaoni zilianza kutungwa tangu Mwaka 2017 na zimeendelea kufanyiwa mamabadiliko Mwaka 2018, 2020, 2021 na 2022 chini ya Sheria ya Epoca.
Marenga anasema sababu kubwa ya kufanyika mabadiliko hayo pamoja na mambo mengine ni kuwa mawasiliano ya mtandaoni ambayo yanatumia maudhui hayo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari, lakini hata hivyo mabadiliko hayo ya kanuni yamekuwa kikwazo kikubwa kwa haki ya kuwasiliana na uhuru wa vyombo vya habari nchini.