Serikali ya Tanzania na China zimesisitiza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati ili kuendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.
Msisitizo huo umetolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 7 Mei, 2024.
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kujadili utekelezaji wa maazimio na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na wakuu wa nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan iliyofanyika nchini China mwezi Novemba 2023.
Aidha, wameainisha maeneo mbalimbali ya kimkakati ambayo nchi hizo mbili zimedhamiria kuziendeleza na kuzisimamia kwa maenedeo ya watu wake. Maeneo hayo ni pamoja na kuanzisha na kuimarisha ushirikiano wa miji dada, kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji, ujenzi wa miji ya kisasa, maendeleo ya viwanda, kilimo cha kisasa na uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo na mifugo na kuboresha mradi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Kwa upande wake Waziri Makamba ameeleza kuwa Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na China ambapo kwa uchache alitaja baadhi ya maeneo ambayo Tanzania imekuwa ikinufaika na ushirikiano huo kama vile; ushirikiano kati ya Jeshi la Ulinzi la Tanzania na China uliodumu kwa zaidi ya miaka 60.
Kuongezeka kwa muingiliano wa wananchi wa pande hizo mbili kumepelekea kukua kwa shughuli za kiuchumi hususan katika sekta ya biashara, usafirishaji na utalii.
“Tanzania imijiweka mikakati thabiti ya kuyafikia maendeleo ya viwanda, hivyo imeweka kipaumbele cha kufanikisha hilo kupitia ushirikiano wake na China” Waziri Makamba
Naye Balozi wa China nchini ameeleza kuwa China itaendeleza ushirikiano wake wa kihistoria na Tanzania ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini kwa ufanisi.
Sekta nyingine za ushirikiano kati ya Tanzania na China ni pamoja na elimu, afya, kilimo, biashara, uwekezaji, kilimo, utalii, nishati, madini, usafirishaji, mifugo na utamaduni.
Balozi wa China nchini, Mhe. Chen Mingjian akifafanua jambo wakati alipofanya mazungumzo Mhe. Makamba katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es salaam tarehe 7 Mei, 2024. |
Mazungumzo yakiendelea. |