Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani Meja Edward Gowele amewataka watu wote wanaoishi mabondeni na kwenye maeneo yaliyozingirwa na Maji kuondoka na kuhamia kwenye maeneo yaliyotengwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa kupokea misaada mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya milioni 25 kutoka Chama cha Lions Club Tanzania Kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Wilaya ya Rufiji Meja Gowele amesema kuwa serikali itaendelea kutoa maeneo ya kutosha ili kuhakikisha Wananchi wanakuwa sehemu salama.
Meja Gowele amesema serikali kupitia wakakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetoa eneo Muhoro ambapo vimetengwa viwanja 6,000 na vimegawiwa bure hivyo wanaendelea kuhamasisha wananchi watoke katika maeneo hatarishi.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha Lions Club Tanzania Lion Happiness Nkya amesema kuwa miongoni mwa kazi ambazo wamekuwa wakizifanya ni pamoja na kuwasaidia wahitaji wakati wanapopata na majanga, hivyo wameweza kutoa misaada mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya milioni 25 kutoka Chama katika Chama hicho.
Ameziomba Taasisi zingine kuweza kujitokeza na kuwasaidia waathirika hao.
Mratibu wa Misaada na Maafa wa Chama hicho, Muntazir Bharwani amesema kuwa wametoa misaada hiyo ikiwa ni sehemu ya kumuunga Mkono Rais Samia katika jitihada za kuwasaidia Wananchi waliokubwa na Maafa hayo.
Amesema miongoni mwa misaada hiyo waliyoitoa ni Sukari kilo 1,000, mchele kilo 1,000, sembe kilo 1,000, maharage 1,000, mafuta ya kupikia lita 612, Blanketi 8, 000, Foronya 400, mikeka 210, kandambili peya 400, sabuni miraba 400, dawa na vifaa za hudumaya kwanza, nguo za watoto, mbegu za mahindi kwa ajili ya wakulima kila 400 ambapo vina thamani ya shilingi 26, 310, 000.