Serikali imeamua kuboresha uelewa wa somo la Kiingereza kuanzia Shule za msingi darasa la kwanza badala ya kuanzia darasa la Tatu kama hapo awali ili kuwajengea uwezo wanafunzi hao ingali mapema kuelewa somo hilo kwa ueledi.
Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (Elimu) Dkt. Charles Msonde amezungumza hayo na walimu wa wilaya ya Chato na amesema moja ya maboresho ni ufundishaji wa lugha hiyo pamoja na kiboresha mitaala.
Dkt. Msonde amesema hali ya ufaulu wa somo la Kiingereza katika matokeo ya Darasa la Saba mwaka Jana na mwaka juzi siyo ya kuridhisha ndiyo maana Serikali imeamua kuja na mkakati huo.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Charles Msonde amesema ufaulu wa wanafunzi waliofanya mtihani wa kitaifa wa Darasa la 7 mwaka Jana ni asilimia 34 ndiyo waliofaulu somo hilo la Kiingereza wakati lugha hiyo ndiyo msingi wa ufundishaji wa masomo na lugha ya mawasiliano katika Shule za sekondari na matokeo ya mwaka 2022 ufaulu ulikuwa asilimia 29.
Kwa upande mwingine Dkt. Msonde wakati akizungumza amewaondoa hofu walimu hao kuwa changamoto zao Serikali inaendelea kuzitatua.
Afisa Elimu Mkoa wa Geita Anthony Anthony Mtweve amewataka walimu wa wilaya hiyo kupokea maono,maagizo na maelekezo na kuzifanyia kazi ili wapige hatua za kiutendaji.