Wanakijiji wa kijiji cha Siliwiti wilayani Momba wametakiwa kuachana na imani potofu za kishirikina ikiwemo ramli chonganishi pamoja na unywaji wa pombe uliopindukia.
Kauli hiyo imetolewa Mei 07, 2024 na Koplo James Chitukulu wakati akizungumza na wanakijiji hao kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu madhara ya imani potofu za kishirikina na kujichukulia sheria mkononi na kusababisha mauaji pamoja na vitendo vingine vya kikatili.
Koplo James alisema kuwa, unywaji Pombe kupindukia umekuwa na matokeo hasi kwenye jamii ambapo asilimia kubwa ya watu waliojiingiza kwenye matendo hayo wamekuwa wakiishia kwenye mikono ya sheria baada ya kutenda kitendo kiovu kilicho kinyume na sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Unapo kunywa pombe kupita kiasi au unapokuwa mtu wakuamini imani potofu za kishirikina na ramli chonganishi ni lazima utafanya vitendo viovu, kinachotakiwa ni kuacha kabisa vitendo hivyo ili kuepuka kuingia kwenye mkono wa sheria”. Alisema Koplo James
Koplo Jamea aliwataka wanakijiji hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kudhibiti matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina katika maeneo yao.