Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amewataka madaktari bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan walio wasili wilayani hapo kwa lengo la kutoa huduma kwa akina mama wajawazito, magonjwa ya watoto, Usingizi na ganzi, upasuaji pamoja na magonjwa ya ndani kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kuwa kwa kipindi kifupi watakacho kuwepo wanahudumia wananchi wengi zaidi.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo wakati akiwapokea madaktari bingwa Watano ambao ni miongoni mwa madaktari waliopo katika mpango kabambe wa utoaji wa huduma za Kibingwa kwenye Hospitali 184 za ngazi ya Halmashauri zinazofanywa na Madaktari bingwa wa Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye kauli mbiu isemayo “Tumekufikia, Karibu Tukuhudumie” ambapo kwa wilaya ya Ludewa madaktari haonwanatajia kufanya kazi kwa muda wa siku nne.
Sanjari na hilo Bi. Mwanziva amesema mara baada ya kukamilisha siku jizo nne za kutoa huduma atahitaji kupata ripoti ya watu walio hudumiwa na kupatiwa tiba pamoja na idadi ya wananchi watakaobaki katika uangalizi wa madaktari wa wilayani hapo ili kuhakikisha lengo la Dakt. Samia Suluhu Hassan la kufikisha huduma ya kibingwa kwa wananchi limefikiwa kikamilifu.
“Tumekuja kuwapokea kwa upendo mkubwa ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini kazi kubwa aliyo ifanya Mh. Rais katika wilaya yetu kwenye sekta ya afya kwani licha ya kutuletea madaktari bingwa lakini tulipokea zaidi ya Sh. Mil 900 kwaajili ya kuboresha majengo haya ya hospitali ya wilaya yetu”. Amesema Bi. Mwanziva.
Ameongeza kuwa ni matumaini yake kuwa maboresho hayo yataendana na huduma bora kwani licha ya mgonjwa kuhitaji tiba lakini pia wanahitaji kupatiwa faraja na upendo ili aweze kupona.
Aidha kwa upande wake Mganga mkuu wa Wilaya hiyo Stanley Mlay amesema ujio wa madaktari hao una faida nyingi ikiwemo kujengewa uwezo kwa baadhi ya watumishi wa afya wilayani hapo pamoja na wagonjwa kupata huduma ambayo wamekuwa wakiikosa katika vituo mbalimbali vya afya na hospitali ya Wilaya.
“Huwa tunapokea wagonjwa wengine ambao magonjwa yao hayawezi kuhudumiwa na wataalamu wa kawaida bali wataalamu bingwa zaidi hivyo hii ni fursa ya kipekee kwa walio na magonjwa yanayohotaji huduma za kibingwa kujitokeza na kutumia fursa hii”. Amesema Dkt. Mlay.
Gabriel Kinusa ni daktari wa magonjwa ya akina mama, lakini pia ni kiongozi wa msafara wa madaktari hao amesema watatoa huduma hizo kwa masaa 24 kwa kushirikiana na madaktari wa wilayani hapo hivyo amewaomba wananchi wote wenye uhitaji na huduma hizo kujitokeza badala ya kusafiri nje ya wilaya na mkoa kwenda kupata huduma hizo.
Amesema wagonjwa watakaofika kupatiwa huduma hizo watapatiwa kwa gharama nafuu kama ilivyo zoeleka kwa hospitali za serikali na kwa wale walio katika mfumo wa kupatiwa huduma bure kama wazee, akina mama wajawazito pamoja watoto walio chini ya miaka mitano watapatiwa huduma hizo kama ilivyo kawaida.
Hata hivyo kwa upande wao baadhi ya wagonjwa waliofika kupatiwa huduma hospitalini hapo akiwemo Anamaria Mwinuka amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaleta madaktari hao kwani wamekuwa na magonjwa kwa muda mrefu na kushindwa kupata huduma kwa wakati kutokana na kushindwa gharama za kusafiri kwenda kufuata huduma hiyo mkoani na mikoa ya jirani.