Na Victor Makinda Morogoro
Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Morogoro (TANROADS),Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amewataka wananchi na viongozi mbali mbali wa kisiasa mkoani Morogoro, ambao barabara zao zimeharibika kutokana na mvua kubwa za masika, kuwa watulivu kwa kuwa wakala huo umejipanga kikamilifu kukarabati maeneo yote korofi ili yaweze kupitika wakati wakisubiri mvua zikatike wafanye marekebisho makubwa ya miundombinu ya barabara mkoa mzima wa Morogoro.
Mhandisi Kyamba aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake mjini Morogoro kwa lengo la kuelezea mikakati ya TANROADS mkoa wa Morogoro, kukarabati barabara zilizoharibika kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu ya barabara mkaoni hapa.
“Tayari wakandarasi wapo kwenye kila wilaya wakishughulikia maeneo yote korofi ya barabara, wakati huu ambao tunasubiri mvua zikatike ili tuanze marekebisho makubwa ya miundombinu mkoa mzima.” Alisema Mhandishi Kyamba.
Mhandisi Kyamba alisema kuwa wakala huo umekuwa ukichukua hatua za haraka na dharura pindi unapotokea uhabifu mkubwa na barabara kushindwa kupitika akitolea mfano namna walivyoshughululikia ujenzi wa daraja lililosombwa na maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika eneo la Ilonga wilayani Ulanga.
Naye Meneja wa TARURA mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, alisema kuwa, TARURA imeelekeza nguvu zake kukarabati barabara zote ambazo ziko chini ya wakala huo ili ziweze kupitika.
Awali akizungumzia na waandishi wa habari mjini Morogoro, kuhusu ubovu wa miundombinu wilayani Ulanga Mbunge wa jimbo hilo, Salim Alaudin Hasham, aliutaka Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), mkaoani Morogoro kuimarisha miundombinu kwenye jimbo hilo kwa kuwa baadhi ya maeneo jimboni humo hayafikiki kwa urahisi kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.
Hasham alisema kuwa ubovu wa miundombinu jimboni ulanga unasababishia lawama kutoka kwa wananchi wakilaumu mbunge wao kushindwa kufuatilia ukarabati wa miundombinu ya barabara.