Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhia Maiti kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Katavi.
Hayo yamebaishwa leo Mei 06,2024 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akijibu swali namba 254 kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Taska Restituta Mbogo aliyetaka kujua, ni lini Serikali itajenga jengo la kuhifadhia Maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Katavi.
Dkt. Mollel amesema ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi utaanza kutekelezwa kabla ya mwaka wa fedha 2023/24 kuisha na kukamilishwa mwaka wa fedha 2024/25.
“Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 12.9 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi”, ameeleza Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake amegawa magari ya kubebea wagonjwa kwa halmashauri zote nchini na hivi karibuni Mkoa wa Katavi wataongezewa gari la kubea wagonjwa.