Katika muendeleza wa kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii kwa lengo la kuijengea jamii uelewa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, uhalifu na kutokufuata sheria za usalama barabarani Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Charles Bukombe amewataka mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu wa timu za Simba na Yanga kufuata sheria za usalama barabarani wanapotumia vyombo vya moto ili kuepuka ajali.
Hayo ameyasema katika uzinduzi wa tawi la Yanga lililipo eneo la Chimbuya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Mei 05, 2024 alipohudhuria hafla hiyo kama mgeni rasmi.
“Madereva hakikisheni mnapopata kibali cha muda kwa ajili ya kusafirisha mashabiki wa Yanga au Simba fikeni kituo cha Polisi kwa ajili ya ukaguzi wa magari yenu kabla ya kuanza safari ili kujihakikishia safari yenu” alisema SSP Bukombe.
Pia aliongeza kwa kusema “Mashabiki acheni kutumia vilevi mkiwa safarini mnapoenda kushangilia timu zenu kwani imebaini kuwa ndio chanzo cha kuwachochea madereva kuwa waongeze mwendo ili muwahi kufika hali inayosababisha Dereva kutofuata sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali” alisisitiza SSP Bukombe.
Aidha, SSP Bukombe amewataka madereva na wananchi wote Mkoa wa Songwe kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika katika jamii na kuharibu miundombinu ya barabara.
Timu ya Yanga ni kati ya timu kubwa na kongwe katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati ikiwa na mashabiki wengi huku ikiwa na historia nzuri katika mashindano ya ndani na kimataifa.