KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akizungumza huko Afisini kwake Kisiwandui Zanzibar.
………
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amewatakia mtihani mwema wanafunzi wote wa kidato cha sita katika mtihani wao wa Taifa.
Kauli hiyo ameitoa katika mahojiano maalum huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, amesema Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinatarajia wanafunzi wote wanaofanya mtihani vizuri na kupata alama za juu za kufaulu ambazo ndio msingi wa kupatikana kwa vijana mahiri na wenye uwezo mzuri wa kukabiliana na masomo ya elimu ya juu.
Katika maelezo yake Mbeto,amewasisitiza kuwa wanafunzi hao kuwa watulivu,majasiri na makini katika kufanya mtihani huo ambao ni chimbuko la kupima uwezo wao wa kitaaluma juu ya masomo yao ya kila siku.
“Chama Cha Mapinduzi kinawatakia mtihani mwema wanafunzi wote wanaofanya mtihani hapa nchini, kumbukeni Serikali,wazazi,walezi na walimu wenu waliotumia muda mwingi kukuandalieni mazingira rafiki ya kujifunza na kusoma wapo pamoja nanyi na walipeni imani ya kufaulu vizuri.”, alisema.
Amesema CCM inaamini maendeleo endelevu ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla yataimarika zaidi kutokana na uwepo wa vijana wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma waopitia katika ngazi mbalimbali za kielimu kwa ajili ya kuandaliwa kuwa wataalamu,viongozi na watendaji wa sekta muhimu nchini.
Mbeto, alisema jumla ya watahiniwa 113,504 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha sita katika shule 931 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea ni 258 katika mchanganuo huo watahiniwa wa shuleni ni 104,449 na watahiniwa wa kujitegemea ni 9,055.
Pamoja na hayo alitoa wito kwa kamati za mitihani,wasambazaji,wamiliki wa skuli,wasimamizi wa mitihani,wazazi,walezi na watahiniwa wote kufuata miongozo ya Necta ikiwa ni sehemu ya kuimarisha amani na utulivu kwa kuepuka changamoto zinazoweza kuharibu mchakato huo.