Katibu Mkuu kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha leo.
 Rais wa Mtandao huo nchini Tanzania , Xavier Daudi akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha leo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakiwafuatilia mada mbalimbali mkoani Arusha .
……………………… 
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, Mhandisi Zena Said amezindua rasmi mtandao wa mameneja rasilimaliwatu katika utumishi wa umma barani Afrika ,tawi la Tanzania (TPSHRMNET) mkoani Arusha .
Akizungumza kwenye  uzinduzi huo ,Zena amesema kuwa uwepo wa mtandao  huo barani Afrika itasaidia sana kukutana na kuangalia changamoto ya rasilimali watu katika sekta ya umma barani Afrika.
Amesema kuwa, kukutana kwao  mkoani Arusha katika mkutano wao sambamba na kuzindua  mtandao huo utasaidia sana kuboresha utendaji kazi wao mahala pa kazi sambamba na kuimarisha juhudi za utoaji haki kwa nchi za Afrika .
“Ili kuhakikisha kila kitu kinaenda  sawa katika kazi zetu ni lazima swala la rasilimali watu lipewe  kipaumbele na kuendelea  kusimamiwa  vizuri sambamba na kutoa elimu kwa wananchi ili kuepuka migongano isiyo ya lazima .”amesema Zena.
Aidha amewataka mameneja rasilimaliwatu kuhakikisha wanasimamia dhana ya serikali mtandao na kutatua changamoto huku wakihakikisha wanarahisisha utoaji wa huduma kwa watanzania ili wafanye vizuri zaidi kwenye maswala ya Tehama.
Hata hivyo amewataka mameneja hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu  mkubwa sambamba na kuwa wazalendo katika utendaji kazi  wao wa kila siku  huku akiwataka kuacha majungu  na uzushi katika maeneo yao ya kazi.
“Nawaombeni sana msiwadharau wale mnaowaongoza kutokana na vyeo  vyenu tendeni  haki na msikilize changamoto zao na kuzifanyia  kazi kwa wakati tuache  kuchafuana kila  mmoja atimize wajibu wake kwa wakati “amesema .
Hata hivyo amewataka mameneja  hao kuondokana na wizi wa fedha kwenye taasisi zao kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifanya wizi kwa kuwaibia watumishi wanaowaongoza haki za watu.
Naye Rais wa Mtandao huo nchini Tanzania , Xavier Daudi amesema lengo la kuzindua mtandao huo ni kuweza kubadilishana uzoefu na kuhakikisha bara la Afrika linakuwa na maafisa wenye sifa katika utendaji kazi wao.
Daudi  amesema kuwa,kupitia mtandao huo wataweza kuhamasishana kama Luna teknolojia yoyote mpya wataweza kutumia fursa kuhimizana katika matumizi yake sambamba na kubadilishana uzoefu baina ya nchi na nchi.
“Tunaendelea kusisitiza sana kuwepo kwa matumizi ya Tehama huku tukiwataka wataalamu wetu kwenda na kasi ya teknolojia, na tunahitaji  watu waliobobea kwenye utalaamu na ili hayo yote yatokee  lazima kuwepo na ubora katika kada hiyo  rasilimali watu .’amesema.
Mmoja wa washiriki katika mkutano huo Gloria Mboya amesema kuwa,watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa katika kutimiza malengo yao na kuahidi  kuyafanyia kazi yale maelekezo yote yaliyotolewa  na Waziri.