………………………
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Said amezindua rasmi mtandao wa mameneja rasilimaliwatu katika utumishi wa umma barani Afrika ,tawi la Tanzania (TPSHRMNET) mkoani Arusha .
Akizungumza kwenye uzinduzi huo ,Zena amesema kuwa uwepo wa mtandao huo barani Afrika itasaidia sana kukutana na kuangalia changamoto ya rasilimali watu katika sekta ya umma barani Afrika.
Amesema kuwa, kukutana kwao mkoani Arusha katika mkutano wao sambamba na kuzindua mtandao huo utasaidia sana kuboresha utendaji kazi wao mahala pa kazi sambamba na kuimarisha juhudi za utoaji haki kwa nchi za Afrika .
“Ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa katika kazi zetu ni lazima swala la rasilimali watu lipewe kipaumbele na kuendelea kusimamiwa vizuri sambamba na kutoa elimu kwa wananchi ili kuepuka migongano isiyo ya lazima .”amesema Zena.
Aidha amewataka mameneja rasilimaliwatu kuhakikisha wanasimamia dhana ya serikali mtandao na kutatua changamoto huku wakihakikisha wanarahisisha utoaji wa huduma kwa watanzania ili wafanye vizuri zaidi kwenye maswala ya Tehama.
Hata hivyo amewataka mameneja hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu mkubwa sambamba na kuwa wazalendo katika utendaji kazi wao wa kila siku huku akiwataka kuacha majungu na uzushi katika maeneo yao ya kazi.
“Nawaombeni sana msiwadharau wale mnaowaongoza kutokana na vyeo vyenu tendeni haki na msikilize changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa wakati tuache kuchafuana kila mmoja atimize wajibu wake kwa wakati “amesema .
Hata hivyo amewataka mameneja hao kuondokana na wizi wa fedha kwenye taasisi zao kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifanya wizi kwa kuwaibia watumishi wanaowaongoza haki za watu.
Naye Rais wa Mtandao huo nchini Tanzania , Xavier Daudi amesema lengo la kuzindua mtandao huo ni kuweza kubadilishana uzoefu na kuhakikisha bara la Afrika linakuwa na maafisa wenye sifa katika utendaji kazi wao.
Daudi amesema kuwa,kupitia mtandao huo wataweza kuhamasishana kama Luna teknolojia yoyote mpya wataweza kutumia fursa kuhimizana katika matumizi yake sambamba na kubadilishana uzoefu baina ya nchi na nchi.
“Tunaendelea kusisitiza sana kuwepo kwa matumizi ya Tehama huku tukiwataka wataalamu wetu kwenda na kasi ya teknolojia, na tunahitaji watu waliobobea kwenye utalaamu na ili hayo yote yatokee lazima kuwepo na ubora katika kada hiyo rasilimali watu .’amesema.
Mmoja wa washiriki katika mkutano huo Gloria Mboya amesema kuwa,watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa katika kutimiza malengo yao na kuahidi kuyafanyia kazi yale maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri.