Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Mwalimu Hasan Elias Masala amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kununua na kuzisimika taa eneo linalozunguka uwanja wa CCM Kirumba na shule ya msingi Kitangiri linalokabiliwa na changamoto ya uwepo wa biashara ya ngono kwa madada na makaka poa nyakati za usiku
Akizungumza katika ziara yake ya kawaida katika kata ya Kitangiri viwanja vya shule ya msingi Kitangiri, Mhe Masala amempongeza Mbunge huyo pamoja na kuitaka manispaa ya Ilemela kuhakikisha inaunga mkono jitihada hizo za Mbunge kwa kununua na kuzifunga taa nyengine Tano ili eneo lote la shule za Kitangiri kuwa salama
‘.. Mbunge ameona changamoto hii na akaamua kununua taa na kuzifunga, Sasa wajibu wetu kama halmashauri na sisi tununue taa nyengine Tano ili eneo hili liwe na mwanga hawa madada poa waondoke, watoto wetu hawawezi kuwa salama kama wana muingiliano na watu wengine wasiokuwa wema ..’ Alisema
Aidha Mhe Masala ameitaka manispaa ya Ilemela kuanza mara Moja ujenzi wa uzio wa shule za msingi Kitangiri pamoja na kuzitaka nyumba za kulala wageni zilizo jirani na eneo hilo kuzingatia na kufuata sheria kwa kutojihusisha na biashara za ngono na kwamba wakiendelea kukaidi agizo hilo Serikali haitosita kuzifungia nyumba hizo za wageni
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula, Ndugu Charles David Karoli mbali na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa fedha za miradi ya maendeleo na Mkuu huyo wa wilaya Kwa kazi nzuri ya kusimamia fedha hizo amesema kuwa Mbunge amekuwa akitatua kero mbalimbali zinazokabili wananchi wake na kwamba mbali na kutoa taa hizo atatoa matofali ya kujenga zahanati ya Kitangiri kati na jiwe kuu mara baada ya wananchi wa maeneo hayo watakapoanza zoezi la ujenzi
Nae Mwenyekiti wa CCM kata ya Kitangiri amesema kuwa chama chake kinaridhishwa na kazi nzuri zinazofanyika na kwamba utekelezaji wa shughuli hizo za maendeleo utasaidia kazi ya uchaguzi kuwa nyepesi kwani chama chake kitashinda Kwa kishindo
Akihitimisha diwani wa kata ya Kitangiri Mhe Donald Ndaro ameishukuru Serikali Kwa utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kwamba anaungana na viongozi wengine katika kuendelea kusukuma mbele maendeleo kwa wananchi wake