MWENENDO WA KIMBUNGA “HIDAYA” KATIKA BAHARI YA HINDI MASHARIKI MWA PWANI YA TANZANIA
Dar es Salaam, 04 Mei 2024 saa 10:00 Jioni:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” katika maeneo ya pwani ya nchi yetu. Mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” unaonesha kuwa mnamo saa 3 asubuhi ya leo, kimbunga hicho kimepoteza nguvu yake kwa kiasi kikubwa wakati kikiingia nchi kavu katika kisiwa cha Mafia.
Aidha, mawingu ya mvua yaliyokuwa yakiambatana na kimbunga hicho yamesambaa katika maeneo ya kusini mwa nchi hususan katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na maeneo jirani na kuweza kusababisha vipindi vya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo. Kwa mafano hadi kufika saa 9 mshana, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 200.8 kwa kipindi cha masaa 6 yaliyopita. Kiwango hiki cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu. Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 6 katika kituo hicho ni takribani asilimia 208 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko.
Kwa upande mwingine, katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam vipindi vya upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa vimeendelea kujitokeza katika nyakati tofauti hadi kufika saa 9 mchana wa leo.
USHAURI: Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na athari zake hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanza