Mkuu wa Idara ya Huduma za Kadi na Malipo wa Exim Bank, Paritosh Babla (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Mgahawa wa Chef’s Pride, Salim Mahsen Al Amry, wakisaini makubaliano ya ushirikiano katika uzinduzi rasmi wa tawi la Chef’s Pride Dodoma. Kupitia ushirikiano huu, wateja wa Benki ya Exim watapokea ofa mbalimbali na punguzo wanapofanya malipo kwa kutumia kadi zao za Exim Bank. Tukio lilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary S. Senyamule, kama Mgeni Rasmi.
……………………..
(Dodoma, 4 Mei 2024). Katika kuendeleza ushirikiano na wateja wake, Exim Bank imeingia makubaliano na Mgahawa wa Chef’s Pride ikiwa ni pamoja na kutoa punguzo na ofa mbalimbali kwa wateja wake watakaotumia kadi za benki hiyo kufanya miamala ya malipo. Tukio hili pia liliambatana na uzinduzi rasmi wa mgahawa wa Chef’s Pride uliofanyika jijini Dodoma.
Hafla hiyo iliyoudhuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule kama Mgeni Rasmi, ilifanyika jijini Dodoma ambapo Mhe. Rosemary aliwapongeza Exim Bank mashirikiano hayo.
“Serikali tunawapongeza benki ya Exim kwa maamuzi yao ya kuja kuwekeza Dodoma kama sehemu ya kusogeza huduma kwa wateja wao popote pale walipo. Tunahimiza na kuwakaribisha wawekezaji wengine kuiga mfano huu wa Exim Bank,” alisema Mhe. Rosemary.
Akizungumzia mashirikiano hayo, Meneja Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano Wa Exim Bank, Bi. Kauthar D’souza alisema, “Benki ya Exim tumekuwa na kawaida ya kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora za kifedha kwendana na mabadiliko ya kidijitali yanayotokana na maendeleo ya teknolojia. Tunafuraha kubwa kuungana leo na mgahawa wa Chef’s Pride katika kuboresha huduma zetu kwa wateja hasa matumizi ya kadi za benki yetu.”
Ushirikiano huu pia unalenga kukuza urahisi na usalama wa miamala ya wateja wa benki hiyo. Halikadhalika, ushirikiano huu ni mwendelezo wa jitihada za benki ya Exim kuongeza matumizi ya kufanya miamala kupitia kadi zao ili kuwapa fursa wateja wake kufurahia ofa mbalimbali pamoja na punguzo. Pia, kwa yule ambaye hana akaunti na Exim Bank anaweza kutembelea tawi lolote la Exim na kupata kadi yake ya malipo ya kabla (Prepaid) ili kuweza kufurahia ofa hii.
Kupitia huduma hii, mteja ataweza kutumia kadi yake kufanya miamala ya malipo na kupata punguzo maalumu na ofa zingine utakapofanya miamala ya malipo kwa kutumia kadi yetu.
Akielezea baadhi ya ofa hizo, Kauthar alisema, “Wateja watakaowahi kupata kadi za Exim bank na wale watakaotumia fedha zaidi wataondoka na zawadi za vocha na kadi za malipo ya kabla yenye fedha ndani yake.”
Exim Bank imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini katika sekta kadhaa kama vile uchumi, uwezeshaji, elimu, afya, mazingira, usalama, na teknologia kupitia sekta binafsi pamoja na serikali ya Tanzania.