* Awahimiza Wachungaji kuwa na Maono Makubwa
*Awataka kuhubiri amani na upendo
* Awahimiza kumtia moyo Rais Samia kutekeleza miradi ya maendeleo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewashauri wachungaji kuwa na maono makubwa katika kuongoza waumini katika makanisa yao ili kujenga Taifa la watu wenye mwelekeo chanya.
Akizungumza leo (Mei 3, 2024) Jijini Dodoma wakati wa kufunga kikao cha mazungativu (Retreat) kwa wachungaji wa Kanisa la FPCT, Dkt. Biteko amesema kuwa ili waumini wapate uelekeo wa kwenda mahali fulani, wanahitaji mtu mmoja miongoni mwao atakaye waongoza kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na maono aliyonayo.
“Wachungaji msihangaike na wingi wa watu mahali popote, angalia uwezo wa kiongozi anayeona mbali atawaongoza wafike mbali”, amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa “ Askofu Mkuu umechagua fungu jema kufanya wachungaji hawa wakutane hapa kujiongezea maarifa kwa kuwa tuko katika dunia iliyojaa utandawazi na mafundisho ya kweli na yasiyo ya kweli. Ni vigumu kwa waumini kutambua ya kweli na yasiyo ya kweli hivyo, wanahitaji kuongozwa”.
Aidha, Dkt. Biteko amewahimiza viongozi wa dini kuwaongoza waumini kiroho na kuchagua viongozi sahihi wanaofahamu kuwa watawaletea maendeleo na ustawi wa nchi.
Pia, amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini kufanya kazi kwa bidii, kuhubiri kuhusu amani pamoja na kusisitiza maadili kwa waumini.
Dkt. Biteko ametaja mafanikio mbalimbali ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, huku akiwaomba wachungaji hao kuendelea kumuombea na kumtia moyo ili aendelee kutekeleza miradi ya nchi katika maeneo mbalimbali.
“ Mradi wa reli ya kisasa (SGR) ni mradi mkubwa haikuwa rahisi kupata fedha za kutekeleza mradi huu lakini Rais Samia amefanikiwa, Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere unaozalisha megawati 2115 umefanikiwa, Pia Serikali imejenga madarasa, zahanati, vituo vya afya na kutoa ajira kwa watumishi wa sekta ya afya, angalieni nia yake, muungeni mkono”, amebainisha Dkt. Biteko.
Vilevile, amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa dini na imani za watu hivyo viongozi wa dini wahimize waumini kuchagua viongozi wanaofaa
“Mwaka huu tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, viongozi wa dini mna uwezo wa kuwahamasisha waumini waweze kuchagua viongozi wanaowahitaji kwa ajili ya kuwaletea maendeleo”, amesisitiza Dkt. Biteko.
Naye, Askofu Mkuu wa FPCT, Steven Mulenga amesema kuwa lengo la semina hiyo ya siku nne kwa wachungaji ni kuwajengea uwezo watumishi wa Mungu namna ya kumkaribisha Yesu Kristo.
“ Haya tuliyofundishana yatakuwa na matokeo kwa nchi ya Tanzania”, amesema Askofu Mulenga.
Semina hiyo wa wachungaji FPCT imehudhuriwa na wachungaji kutoka nchi za Kenya, DRC, Rwanda na Sudani Kusini.