Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amebainisha mikakati ya serikali katika kuongeza uzalishaji wa zao la Mkonge kutoka tani 56,732.69 mwaka 2023/2024 hadi tani 80,000 mwaka 2024/2025.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka 2024/2025, Mhe. Bashe amesema Wizara yake kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) lengo hilo litafikiwa kwa kununua zana za kilimo kwa ajili ya kuwezesha uendelezaji wa mashamba makubwa ya pamoja na kununua mashine ya kuchakata mkonge (korona).
“Pamoja na mambo mengine, tutaendeleza miundombinu ya kituo cha uchakataji cha Handeni, kukarabati miundombinu ya shamba la Kibaranga na kuwezesha umiliki wa ardhi ya kilimo yenye ukubwa wa hekta 6,000 kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja katika mikoa ya Tanga, Singida na Morogoro.
“Aidha, Bodi itaratibu usambazaji wa miche ya Mkonge milioni tatu katika maeneo ya uzalishaji na kupitia TARI itatoa mafunzo kuhusu uzalishaji wa Mkonge na fursa zitokanazo na zao hilo kwa wadau 100,000 na maafisa ugani 500,” amesema Mhe. Bashe.
Mhe. Bashe amesema katika kuongeza matumizi ya mmea wa Mkonge, Bodi kwa kushirikiana na Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST), itajenga kituo cha uzalishaji wa Inzi chuma (black soldier flies) kwa kutumia mabaki ya Mkonge (Sisal waste) ili kutengeneza protini kwa matumizi ya binadamu na mifugo (wanyama, ndege na samaki).
“Pia, Bodi itawezesha utafiti wa zao la Mkonge utakaofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), TARI-Mlingano, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) kwa kushirikiana na Kampuni ya Carbonovia UK ya Oxford Uingereza kuhusu uwezekano wa kuzalisha protini kutokana na hewa ukaa (Carbon dioxide) kutoka kwenye mabaki ya Mkonge.
“Aidha, Bodi kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na Chuo cha Mafunzo Zanzibar itaanzisha na kuimarisha utaalamu wa uzalishaji wa bidhaa za mikono za Mkonge ili kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake,” amesema Mhe. Bashe.