Na Adeladius Makwega- MWANZA
Umoja wa Wanafuzi Wakatoliki wa Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu Tanzania(TMCS) umewataka wanachama wake kuhakikisha wanatoa michango yao kwa wakati na kwa kufanya hivyo watasaidia umoja wao kutimza majukumu yake ya kila siku na
wanachama watakuwa wametimiza wajibu wao kwa chama na kwa Mungu.
Hayo yamesemwa jioni ya Mei Mosi, 2024 katika viunga vya Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya na Mtunza Fedha wa umoja huo Kanda ya Mwanza Bi. Merina Pascal wakati akizungumza na wanachama wa tawi la chuo hiki alipotembelea kufuatilia
maendeleo ya uhai wa tawi hilo.
“Tupo hapa kwenu, tunawakumbusha kutoa michango yote kama ilivyo ili kusaidia viongozi wenu kupata moyo wa majukumu haya ya kiimani ili waweze kuwaongoza vema.”
Katika ziara hiyo Bi. Merina Pascal aliambatana na Mhazini Msaidizi TMCS Jimbo ndugu Robert Mlay na miongoni mwa majukumu waliyofanya ni kusimamia uchaguzi wa viongozi wa tawi hilo.
Katika uchaguzi huo viongozi kadhaa walichaguliwa; “Abrahamu Engidongi Rundo (Mwenyekiti) Francis Lukas Maramonyi (Makamu Mwenyekiti) Alphonce Sadock (Katibu) Mariamu Kabanya Seleli(Katibu Msaidizi) Francis Joachim Panga(Mhasibu).
Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo Mwenyekiti wa tawi la TMCS Malya Abrahamu Rundo ameshukuru kwa kuchaguliwa, akitoa ahadi kuwa hatowaangusha huku akiomba ushirikiano kwa kila mwanachama.
Kwa upande wake Mkufunzi Mlezi TMCS tawi hilo Denis Kayombo alisema kuwa anawapongeza wanachama wote waliochaguliwa kwa nafasi zote na anawapongeza pia wale waliopiga kura, “Kikubwa kwenu tambueni kuwa TMCS pia ni pahala pakujifunza uongozi, mvumiliane kila mmoja na madhaifu yake, viongozi ni binadamu na hata wapiga kura ni binadamu pia.
Uongozi wa dini siyo wa kuukwepa kesho unaweza kusimama sehemu ukasema ‘Jamani mimi nilikuwa kiongozi TMCS pale Malya.’ Hilo likafanya wewe uaminike, fanyeni kazi kwa bidii na moyo wote.”
TMCS ni Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki wa Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu Tanzania ambapo ulianzishwa mwaka 1984 pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo wazo hilo likakuzwa zaidi mwaka 2006 kwa kuhusisha vyuo kadhaa na mwaka 2009 wakichaguliwa viongozi wa umoja huo.
TMCS inatokana na Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Ulimwenguni (IMCS) ambao ulianzishwa mwaka 1921 huko Fribourg Uswiswi.