Na WAF – Dar Es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimy amebainisha kuwa takribani wagonjwa wapya wa Saratani 40,000 hugunduliwa kila mwaka na karibu jumla ya watu 27,000 wenye Saratani hufariki dunia nchini Tanzania.
Waziri Ummy amesema hayo leo Mei 2, 2024 kwenye uzinduzi wa jengo la huduma za Saratani lililopo Hospitali ya Aga Khan iliyozinguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambapo kituo hicho kitatoa huduma kwa wagonjwa 100 kwa siku.
“Takwimu za ufuatiliaji wa Saratani kupitia ripoti ya utafiti ya Globocan zinaonesha kuwa nchini Tanzania takribani wagonjwa wapya wa Saratani elfu 40 hugunduliwa kila mwaka na karibu jumla ya watu elfu 27 wenye Saratani hufariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.” Amesema Waziri Ummy
Amesema, sehemu kubwa ya wagonjwa wa Saratani hapa nchini wamebainika kuwa ni wanawake wenye Saratani ya mlango wa kizazi ambapo Saratani hii pekee inachangia 25% ikifuatiwa na Saratani ya matiti kwa 10% ambapo kwa pamoja Saratani hizi zinachangia zaidi ya 33% ya wagonjwa wote na kwa pamoja zinachangia karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na Saratani hapa nchini.
“Vifo vitokanavyo na Saratani vitaongezeka ifikapo mwaka 2030 kama hatutachukua hatua za kushuhulikia ukubwa wa tatizo hili la Saratani nchini ambapo inakadiriwa kufikia vifo Milioni Moja kwa Mwaka 2030.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na mapambano dhidi ya Saratani ambapo amesema fedha imepatikana ya kuboresha miundombinu, ununuzi wa vifaa vya kisasa pamoja na kusomesha wataalam katika matibabu ya Saratani.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Samia ametupatia Bilioni 10 Mwaka huu, tumesomesha madaktari bingwa na bozezi kwenye masuala ya Saratani zaidi ya 30 ambao tumewapeleka nje ya nchi ambao watakuja kusaidia kupunguza tatizo la Saratani nchini.” Amesema Waziri Ummy