Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,Wakili Kihomoni Kibamba akionesha nyaraka mbalimbali zenye orodha ya majina ya wafanyabiashara pamoja na makampuni ya maegesho ambao hawalipa kodi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Kihomoni Kibamba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
……..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetoa siku nne kuanzia Mei 2 hadi Mei 5 mwaka huu kwa wafanyabiashara Jijini humo kulipa ushuru,kodi na ada mbalimbali kwa hiari.
Siku hizo zimetolewa baada ya uongozi wa Halmashauri hiyo kuona wafanyabiashara hao wakisuasua katika ulipaji wa tozo hizo licha ya jitihada mbalimbali ambazo wameishazifanya ikiwemo kutumia watendaji wa mitaa pamoja na magari ya matangazo kutangaza kwa ajili ya kuwakumbusha na kuhamasisha lakini hawakufaya hivyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Mei 2, 2024 na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Wakili Kihomoni Kibamba wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake.
Amesema kutokana na bajeti yao wanatakiwa kukusanya takribani bilioni tano kwenye vyanzo mbalimbali ambapo kodi hizo zinaiwezesha Halmashauri hiyo kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwamujibu wa sheria.
“Mwaka wa fedha unaisha Juni 30 mwaka huu katika miezi hii miwili tumejipanga kuhakikisha kila Senti inayopaswa kukusanywa inakusanywa pasipo kupoteza hata senti moja,hivyo wafanyabiashara msisubili hadi tuchukue hatua ambazo hazitawafurahisha”, amesema Wakili Kibamba
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanalipia Kodi zote kwenye mifumo ya kielektroniki ili kuepuka usumbufu utakaoweza kujitokeza ikiwemo ya kutotambulika kwa malipo.