Mwenyekiti wa AAPAM Tanzania Chapter, Leila Mavika akizungumza kuhusiana na mkutano huo.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejiment ya utumishi na utawala bora,George Simbachawene akifungua mkutano huo mkoani Arusha leo.
Washiriki mbalimbali wa mkutano huo wakimsikiliza Waziri Simbachawene katika mkutano huo mkoani Arusha leo .
………….
Happy Lazaro,Arusha .
WAKUU wa idara wanaosimamia utawala na rasilimali watu katika utumishi wa umma wametakiwa kuhakikisha wanasimamia ipasavyo watumishi wao wanaowasimamia ikiwemo kushughulikia changamoto zao kwa wakati na kwa kutenda haki.
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na ,Waziri wa nchi ofisi ya Rais menejiment ya utumishi na utawala bora,George Simbachawene wakati akifungua mkutano wa 11 wa mwaka wa wanachama wa( AAPAM) tawi la Tanzania na uzinduzi wa jumuiya ya maafisa tawala na Rasilimali watu Tanzania (TAPAHR) unaofanyika mkoani Arusha kwa muda wa siku tatu.
Amesema kuwa , kumekuwepo na changamoto ya maafisa hao kutosimamia ipasavyo watumishi wao kitendo ambacho changamoto yoyote ikitokea wamekuwa wakikimbilia kwa viongozi wa ngazi za juu ili waweze kupata haki zao kitendo ambacho hakitakiwi tena.
“Nawaombeni sana mkafanye kazi mliyopewa katika maeneo yenu katika kuhakikisha mnasilikiza changamoto za watumishi wenu na kuzitatua kwa wakati badala ya kuzipuuzia na kusababisha kwenda kulalamika ngazi za juu wakati nyie mpo na mmeajiriwa kwa kazi hiyo”amesema Simbachawene.
“Wakati mwingine mtumishi anapokuja kulalamika na changamoto yake kwako unatakiwa umsikilize hoja yake na sio kukimbilia kumwadhibu bila ya kujua changamoto yake kwani wengine wanahitaji ushauri tu kutokana na changamoto wanazopitia na sio kuwachukulia hatua haraka haraka na hayo siyo maadili ya utumishi.”amesema .
Simbachawene amesema kuwa,kumekuwepo na changamoto kubwa ambayo imekuwa ikijirudia kwa baadhi ya watumishi kwenda kwa viongozi ngazi za juu kueleza changamoto zao kutokana na viongozi wanaowasimamia kushindwa kuwasikiliza na kuangalia namna ya kuzitatua,tunaomba sana hilo lisijirudie tena kila mmoja atekeleze wajibu wake ipasavyo.
Aidha Simbachawene amewataka maafisa hao kutumia nafasi zao kukutana na watumishi wao mara kwa mara na kuweza kuwakumbusha sheria za kiutumishi pamoja na kuwajengea uelewa juu ya mifumo mbalimbali ya utumishi kwani wengi wao hawajui sheria .
Hata hivyo amewataka watumishi hao kusimamia ipasavyo mfumo wa usimamizi wa utendaji kazi katika utumishi wa umma (PEPMIS) na endapo watajulikana kukiuka sheria hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaobainika kuchezea mfumo huo wa serikali .
“Natumia fursa hii kuwakata watumishi wote kujiunga na mfumo huo wa kwani ni muhimu sana kwao kuweza kuweka kumbukumbuku za utendaji kazi wao na ufanisi katika utendaji kazi na kuweza kupimwa kulingana na utendaji wao kwani kupitia mifumo hiyo ndio kipimo pekee cha mtumishi kuweza kupandishwa cheo na hata Mishahara” amesema .
Naye Kaimu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, Felister Shuli amesema lengo mkutano huo ni kutoa fursa kwa wataalamu wa rasilimali watu kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu utawala na rasilimali watu sambamba na kupitia changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzifanyia kazi.
Shuli amesema kuwa ,mada mbalimbali zitakazotolewa katika mkutano huo ni sehemu ya kuongeza ufanisi na taaluma zaidi katika maeneo yao ya kazi .
Kwa upande wake Mwenyekiti wa AAPAM Tanzania Chapter, Leila Mavika amesema kuwa, kauli mbiu ya mwaka huu ni “usimamizi wa utendaji kazi katika utoaji huduma,nafasi ya Tehama katika kuimarisha utendaji kazi katika utumishi wa umma.”amesema Mavika.
Leila amesema kuwa,jumuiya ilianzishwa miaka 50 iliyopita na makatibu wakuu wanasimamia utawala bora barani Afrika walipokutana kujadili changamoto mbalimbali kupitia mikutano hiyo mnsmo amwaka 1971 wakuu wa utumishi wa umma barani Afrika waliamua kurasimisha rasmi mkutano huo ambao ulizaa rasmi jumuiya hiyo ya barani Afrika ambao ulizaa utawala wa usimamizi wa umma.
Amesema kuwa, walikubaliana kuwa kila mwaka kitakuwa kunafanyika mkutano kwa zamu katika miji mkuu kwa nchi wanachama .
“AAPAM inaongozwa na kamati tendaji baraza na sekretariet ambapo kila mwaka kunakuwa na mkutano unafanyika kila nchi watakavyokubaliana na kuna katiba ambayo inaongoza AAPAM.”amesema .