Mkurugenzi Mtendaji Hospital ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dkt. Paul Sarea akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau wa kuchambua mwonekano wa utekelezaji wa mradi wa afya ya akili kwa vijana ‘Being Mental Health Initiative’ uliofanyika kwenye Hoteli ya Protea Courtyard.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Africa Academy for Public Health (AAPH) Dkt. Mary Sando akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya mradi wa mradi wa afya ya akili kwa vijana ‘Being Mental Health Initiative’ uliofanyika kwenye Hoteli ya Protea Courtyard.
Mtafiti Mwandamizi wa Program ya Africa Academy for Public Health (AAPH) na Mratibu wa Mradi wa Being – Tanzania na Ghana Dkt. Innocent Yusufu akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya mradi wa afya ya akili kwa vijana ‘Being Mental Health Initiative’.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika mkutano wa kuchambua mwonekano wa utekelezaji wa mradi wa afya ya akili kwa vijana ‘Being Mental Health Initiative’ uliofanyika leo Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye Hoteli ya Protea Courtyard.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Africa Academy for Public Health (AAPH) imetoa ripoti ya mradi wa Afya ya Akili kwa vijana ‘Being Mental Health Initiative ambayo imeonesha kuongezeka kwa idadi kubwa ya vijana wenye Changamoto ya afya ya akili, huku taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wemetakiwa kuongeza nguvu kufanya utafiti endelevu juu ya afya ya akili ya vijana zinazolenga kuzuia na kukuza afya ya akili pamoja na kuunda vikundi vya kimkakati vyenye lengo la kujadili na kushauri ili kufikia malengo tarajiwa.
Akizungumza leo Mei 2, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa kuchambua mwonekano wa utekelezaji wa mradi wa afya ya akili kwa vijana ‘Being Mental Health Initiative’ Mkurugenzi Mtendaji Hospital ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dkt. Paul Sarea, amesema kuwa lengo ni kuwanusuru vijana ili waweze kuepukana na madhara ya afya ya akili.
Dkt. Sarea amesema kuwa wakati umefika kwa wadau kuongea nguvu katika kuhakikisha wanapata majibu ya afya ya akili kwa vijana.
“Ili kutokomeza matatizo ya afya akili kwa vijana walezi na wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto katika kuhakikisha wanapata huduma muhimu ikiwemo kuwasaidia wanapopata shida pamoja na kutoa ushauri kwa wakati unapoitajika” amesema Dkt. Sarea.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 asilimia 19 ya watanzania ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 ambapo ni vijana wengi ambao wanaitaji msaada.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Africa Academy for Public Health (AAPH) Dkt. Mary Sando, amesema kuwa lengo la mradi wa “Being Mental Health Initiative” ni kushirikisha matokeo ya kazi ya mwaka mzima iliyofanyika kuelewa masuala ya afya ya akili na mambo yanayochochea changamoto za afya ya akili.
Amesema kuwa matokeo ya kazi ya mradi yamesisitiza mapengo yaliyopo, fursa, na hatua muhimu zinazohitajika kukuza juhudi za kuzuia changamoto na kuimarisha afya ya akili kwa vijana.
Dkt. Sando amesema kuwa kulingana na takwimu za UNFPA za mwaka 2024, zaidi ya 33% ya idadi ya watu wa Tanzania inajumuisha vijana wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24.
Amesema kuwa utafiti uliofanywa nchini Tanzania ulionyesha kwamba unyogovu, wasiwasi, matumizi ya dawa za kulevya, na tendo la kujeruhiwa ni miongoni mwa changamoto za afya ya akili kwa vijana.
“Licha ya ushahidi huu, matokeo haya ni ni sehemu ndogo ya picha kubwa kwani utafiti huu ulifanyika kwa miongoni mwa watu wachache na ulihusisha tathmini katika wakati mmoja tu” amesema Dkt. Sando.
Mradi huu ulichukua njia ya mahusiano kwa ustawi, ukizingatia uhusiano wa kutegemezana kati ya mambo mbalimbali yanayoathiri afya ya akili ya vijana.
“Kazi hii ilihusisha kushirikiana na wadau muhimu kutoka serikalini, taasisi za ufadhili, taasisi za elimu ya juu na utafiti, mashirika ya ndani na kimataifa yasiyo ya kiserikali, vijana, na watu waliopitia changamoto za afya ya akili” amesema Dkt. Sando.
Mradi huu ulifadhiliwa na Grand Challenges Canada (GCC) na kutekelezwa na AAPH nchini Tanzania na Ghana (Chuo Kikuu cha Ghana) kupitia Mtandao wa Africa Research Implementation Science & Education
Lengo la mradi wa Being nchini Tanzania linalenga kupunguza unyanyapaaji na kuendeleza ushirikiano wa wadau mbalimbali pamoja na kutoa wito wa kuendeleza juhudi za pamoja ili kuimairisha afya ya akili kwa vijana na kutatua changamoto wanazozipiti.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kufanya utafiti endelevu juu ya afya ya akili ya vijana; kufanya utafiti wa afua mbalimbali zinazolenga kuzuia na kukuza afya ya akili; kuunda vikundi vya kimkakati kujadili na kushauri wadau mbalimbali kuhusiana na maswala ya afya ya akili.