Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kumchukulia hatua Mhandisi aliye simamia ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mtii Wilayani humo kwa uzembe kushindwa kusimamia kikamilifu mradi huo na kusababisha baadhi ya Majengo kuwa chini ya kiwango.
Ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake alipo tembelea kituo hicho na kubaini moja ya majengo ya kituo hicho kuwa na nyufa hali ambayo inatishia usalama wa wafanyakazi na wananchi wanaopata huduma kwenye kituo hicho ambacho tayari kimeanza kutoa huduma kwa baadhi ya majengo yake yaliyojengwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo hicho.
Mbali na agizo hilo kutaka Mhandisi aliye simamia ujenzi kuchukuliwa hatua mkuu huyo wa wilaya ameagiza pia kumkamata mkandarasi aliye tekeleza mradi huo kwa uzembe wa kujenga mradi chini ya kiwango.
“Siwezi kukukabali uzembe wa aina hii nimekuja hapa kwa zaidi ya mara tatu na mara zote kila nikija simkuti Mhandisi wa Halmashauri anawaacha mafundi peke yao, na huyu mkandarasi aliyekuwa akijenga hapa pia akamatwe popote alipo kwa uzembe huu kama msimamizi mkuu wa miradi kwenye Wilaya ya Same sitakubali hujuma ya aina hii kuendelea”. Alisema mkuu huyo wa Wilaya.
‘Hata kwenye miradi mingine ambayo nimekua nikitembelea nimebaini Mhandisi huwa anakuja siku moja kabla ya ziara zangu na hi inaathiri kasi ya utendaji miradi mingi kuchelewa kukamilika kwakua hakuna ufuatiliaji wa karibu kwa wataalam ambao wanalipwa fedha na serikali kwa ajili ya kazi hiyo”.Alisema mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgebi.
Mradi huo ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mtii umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 500 fedha zilizotolewa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kulenga kuboresha huduma ambapo kwa mujibu wa mkuu wa wilaya kwenye ufuatiliaji amebaini Mhandisi wa Halmashauri ameua na tabia ya kuwaacha mafundi pekee bila usimamizi hali ambayo ndio imesababisha majengo kuwa chini ya kiwango.
Baada ya kukagua mradi huo amefanya mkutano na wananchi wa humo wa kusikiliza kero na malalamiko ya wananchi lakini pia kuwasisitiza wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kutumia haki yao kuchagua na kuchaguliwa.