Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi, John Kambona akizungumzia kuhusiana na huduma mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.
Afisa Tehama kutoka chuo hicho, Kitururu Mndeme akielezea kozi mbalimbali wanazotoa.
Baadhi ya wananchi wakipata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na chuo hicho.
………………………….
Arusha .Chuo cha Bandari Dar es Salaam kimeanzisha kozi mpya ya usimamizi wa moto na usalama mahala pa kazi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na majanga ya moto yanayoweza kutokea kwa kuchukua tahadhari ya haraka.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi, John Kambona wakati akizungumza mkoani Arusha na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa ya kujiunga na kozi hiyo kwani ina manufaa makubwa sana kwao na nchi kwa ujumla.
Amesema kuwa, kozi hiyo inatolewa katika ngazi ya cheti na diploma ambapo wamefikia hatua ya kuja na kozi hiyo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama mahala pa kazi ili athari yoyote inapotokea kuwe na watu wenye uelewa wa kutosha wa namna ya kukabiliana na majanga hayo ya moto kabla hayajaleta madhara yoyote.
“Hii kozi tunayotoa sisi ya maswala ya “moto na usalama ” vyuo vingi havina hivyo tunatoa wito kwa wananchi pamoja na watumishi waliopo katika taasisi na makampuni mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo kwa manufaa yao na usalama katika maeneo ya kazi.”amesema .
Kwa upande wake Afisa uhusiano wa chuo hicho, Edda Mmari amesema kuwa, chuo mbali na kutoa kozi hiyo kimeandaa mitaala 15 ya kozi za mafuta na gesi ambayo inatarajia kuanza mwaka wa masomo 2024/2025 ambapo uwepo wa kozi hiyo utasaidia sana kuwaandaa wataalamu waliobobea na wenye utaalamu wa kutosha katika maswala ya mafuta na gesi.
Mmari amesema kuwa, bado mwitikio wa wanawake kujiunga na kozi mbalimbali chuoni hapo ni mdogo kutokana na dhana iliyopo kuwa kozi za mafuta na gesi ni za wanaume, hivyo ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa zinazotolewa na chuo hicho ili kuweza kupata ajira kwa haraka.
“Pamoja na kuwepo kwa changamoto ya mwitikio wa wanawake wachache kujiunga na kozi mbalimbali bado tunaendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili wanawake wazidi kushiriki kwa wingi katika kozi mbalimbali kama ambavyo tumehamasisha katika kozi za mitambo zinazotolewa katika chuo hicho “amesema Mmari.
Hata hivyo amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kusomea kozi hizo zinazotolewa na chuo hicho ili kuweza kuajirika kwa urahisi kwani wataalamu wanawake waliopo katika fani ya mafuta na moto bado ni wachache.
Naye Afisa Tehama kutoka chuo hicho, Kitururu Mndeme amesema kuwa, chuo hicho pia kimekuwa kikitoa kozi mbalimbali ikiwemo kozi ya usimamizi wa shughuli za meli na Bandari, usimamizi wa shughuli za usafiri majini, usimamizi wa forodha, pamoja na usimamizi wa matengenezo ya vifaa vya kushusha na kupakia dhana nzito.
Mndeme amesema kuwa, wanatoa pia kozi za uendeshaji wa mitambo ya kushusha na kupakia dhana nzito ambapo sifa kubwa ya kujiunga na kozi hizo za mitambo ni leseni ya udereva ikiwa na daraja D.