Afisa Usafirishaji Idara ya udhibiti huduma za usafiri Majini Celina Mokiti akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha .
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Uwakala Tanzania (TASAC) Amina Miruko akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
……..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Watumiaji wa Usafiri wa Majini nchini wametakiwa kujisajili katika Shirika la uwakala wa Meli Tanzania(TASAC) kutokana na wengi kutokufahamu haki zao hivyo kushindwa kupata msaada pale wanapopatwa na matatizo.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Usafirishaji Idara ya udhibiti huduma za usafiri Majini Celina Mokiti wakati akieleza baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika Shirika hilo katika maonyesho ya Usalama na Afya mahali Pakazi yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya mahali Pakazi nchini (OSHA) yanayoendelea Mkoani Arusha.
Hata hivyo amesema kuwa, ni muhimu mteja kufahamu haki zake kwa lengo la kuondoa migogoro kati ya watoa huduma na wateja.
Amesema huduma zinazotolewa na wakala huyo wa Meli nchini (TASAC) ni pamoja na kudhibiti watoa huduma, kudhibiti mawakala wa meli, kudhibiti mawakala wa ugomboaji na uondoshaji mizigo baharini, kudhibiti wakusanyaji na watawanyaji mizigo.
Huduma zingine ni kudhibiti watoa huduma ndogondogo bandarini, kudhibiti wahakiki bandarini, sambamba na kudhibiti wanaotoa leseni, kuhuisha na kufuta leseni, kuweka viwango vya huduma na vigezo kwa watoa huduma.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mwandamizi Shirika la Uwakala Tanzania (TASAC) Amina Miruko, ameeleza kuwa wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha usalama wa abiria, vyombo na mizigo kwa viwango vya kimataifa.
Aidha Miruko amesema kuwa,wana Jukumu la kuhakikisha Usalama wa vyombo vya Usafiri wa Majini lakini pia Jukumu lingine ni kuratibu utafutaji na uokoaji pale inapotokea dharura yoyote.
Ameongeza kwamba licha ya usimamizi huo, wanahakikisha kuwepo kwa vifaa vya uokoaji ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kuwa na vyombo vya ukaguzi kwa lengo la kubaini uharifu.
Amefafanua kuwa, (TASAC) ina majukumu ya kuratibu utafutaji na uokoaji inapotokea dharura, TPA na wadau mbali mbali wa uokoaji huwa wanahusishwa ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Maji Zanzibar (ZMA) ili kuokoa abiria na mali zao.
Aidha ameongeza kuwa ,TASAC kwa kushirikiana na wadau wengine wameungana pamoja katika kutoa mafunzo mbalimbali yahusuyo Usalama na Afya mahali pakazi huku Mratibu mkubwa wa Maonesho hayo akiwa ni OSHA.
Maonesho ya Usalama na Afya mahali Pakazi yalianza Mapema wiki iliyopita mkoani Arusha Katika Viwanja vya General Tyre vilivyopo njiro mkoani Arusha ambapo Kilele chake kilikuwa April 28 mwaka huu huku shughuli za maonesho zikitarajiwa Kuhitimishwa rasmi leo April 30.