Wadau wa afya wa Bohari ya Dawa (MSD) Tanga wamehimizwa kusimamia bidhaa za afya zinazosambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma mkoani humo, ili zitumike kama inavyohitajika ikiwa ni pamoja na kusimamia takwimu ili kuwezesha kufanya maamuzi sahihi juu ya upatikanaji wa bidhaazaafya.
Akifungua kikao cha wadau na wateja wa MSD kanda ya Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Jiji Mhe. James Kaji amesema usimamizi sahihi wa mahitaji na matumizi bidhaa za afya unaiwezesha MSD kuagiza kwa usahihi bidhaa hizo na kuboresha upatikanaji wake kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, amewashauri MSD kuhakikisha utaratibu wa vikao vya mwaka vya wadau unaendelea kwani ni vikao muhimu kwa pande zote mbili, yaani Bohari ya Dawa (MSD) yenyewe na wadau ili kwa pamoja kujadili namna ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.
Kwa upande wake Meneja Kanda ya Tanga Sitti Abdulrahman ameeleza kuwa kwa sasa kanda ya MSD Tanga inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 537, na inasambaza bidhaa za afya mara sita kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD Victor Sungusia ameeleza kuwa vikao vya MSD na wadau wake kuanzia sasa vitakuwa endelevu kila mwaka.
MSD Kanda ya Tanga inahudumia Mkoa ya Tanga, na Wilaya moja ya Same iliyopo mkoa wa Kilimanjaro.