Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
April 30
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa( 2024 ), Godfrey Mzava ameeleza ,Rais Samia Suluhu Hassan yupo tayari na amekuwa na utashi kuhakikisha anashusha raslimali fedha kwa ajili ya kutatua kero za wananchi ikiwemo kusogeza huduma ya maji safi,salama na karibu ya jamii.
Mzava alieleza hayo wakati akikagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa maji , ujenzi wa tanki la maji Lita 50,000 kijiji cha Kidomole , Halmashauri ya Bagamoyo Mkoani Pwani mradi ambao utagharimu milioni 176, umefikia asilimia 90 ,utahudumia kaya 700 zenye wakazi 3,660.
Alieleza kwamba , mradi ni mzuri ,kazi zilizobakia zikamilishwe .
“Maji hayana mbadala,kila siku lazima tuguse maji ,kwa umuhimu huo Rais Samia anaendelea kuboresha miundombinu ya maji , kushusha fedha kwenye miradi ya huduma, kujenga miradi ya maji ilihali wananchi wapate huduma na maji safi ,salama yenye uhakika na karibu na mazingira ya wananchi ili watu wasifuate umbali mrefu “alisema Mzava.
Vilevile Mzava alisisitiza, watendaji kuendelea kumsaidia mh.Rais katika jitihada zake madhubuti za kuwaletea wananchi Maendeleo na kuinua uchumi.
“Miradi yote ya maendeleo isimamiwe na muendelee kushirikiana Chama na viongozi wa Serikali ili mambo yaende vizuri, nimeona ushirikiano ulipo sasa muuendeleze kwa manufaa ya jamii “alieleza Mzava.
Mke wa Rais Mstaafu awamu ya nne Salma Kikwete, alipata fursa ya kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya nchini na kutambulika Duniani kwa weledi wake.
Salma alisema, Rais amejipambanua katika haki,usawa na uwajibikaji katika utawala bora, na kuhakikisha Serikali inatoa fedha nyingi za miradi hivyo watendaji, wabunge washirikiane kusimamia.
Akipokea Mwenge wa Uhuru katika viwanja vya shule ya Msingi Fukayosi, kata ya Fukayosi, Shauri Selenda, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bagamoyo kutoka Halmashauri ya Chalinze, miradi 15 yenye thamani ya sh.Bilioni 13.7 itatembelewa na kukimbizwa urefu wa km.159.7.
Miradi mingine iliyotembelewa halmashauri ya Bagamoyo, ni sanjali na kukagua mradi wa duka la dawa za jamii hospital ya wilaya na mradi wa barabara , Kitongoji cha Benki ,kata ya Dunda.
Pamoja na hayo ,umekagua shughuli za makundi yenye mahitaji maalum na ukatili wa kijinsia, kukagua mradi wa sekta ya barabara ,sekta ya elimu ,afya 2024 na kukagua shughuli za Uhifadhi wa mazingira -uchakataji wa mifuko ya sandarusi.