Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kisongo Aprili 30 2024. Kesho atashiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani- Mei Mosi ambayo kitaifa yanafanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani humo, Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri MKuu Kassim Majaliwa akizungumza na wajumbe wa kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, Mei Mosi kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha. Maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa mkoani humo na Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Deogratius Ndejembi alipokagua maandalizi kuelekea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani – Mei Mosi kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha Aprili 30, 2024, Maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa mkoani humo na Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wengine ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga (kulia) na Rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini(TUCTA),Tumaini Nyamhokya (Wapili kulia) (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………..
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo yatafanyika kitaifa mkoani Arusha.
Amesema hayo leo (Jumanne, Aprili 30, 2024) wakati akikagua maandalizi hayo ambayo yatafanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Jijini Arusha.
“Nimeridhishwa na maandalizi, niwatie shime tukamilishe sehemu iliyobaki, kesho tutakuwa wote, Waziri Mhe. Deogratius Ndejembi yupo na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipo hapa”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaridhishwa na ushirikiano uliopo baina yake na vyama vya wafanyakazi nchini na itaendelea kuwajibika kwa yote muhimu yanayowaguswa wafanyakazi “tunazungumza pamoja na kukiwa na jambo lolote tunashirikishana, muelekeo wetu bado ni mzuri”
Kwa upande wake, rais wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini(TUCTA),Tumaini Nyamhokya ambaye alikuwepo katika maandalizi hayo amesema kuwa kamati za maandalizi zimefanya kazi kubwa sana ikiwemo hamasa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo. “Mpaka sasa maandalizi yote yamefikia asilimia 95, na hizo tano kwa Saa machache zilizobaki tunakwenda kuyamaliza”
Mgeni Rasmi katika Maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.