Na Mwandishi Wetu,
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema Uhusiano na Ushirikiano baina ya nchi ya Tanzania na Urusi haujaanza leo, bali ulianza zamani kipindi cha uongozi wa Mwl. Julius K. Nyerere.
Dkt. Pindi Chana amesema hayo alipokuwa akizungumza katika mhadhara uliofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) leo Aprili 30, 2024 Ubungo, jijini Dar es salaam.
Akizungumzia umuhimu wa mhadhara huo, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema wanafunzi wa sheria kwa vitendo walioshiriki katika mhadhara huo watapata faida kubwa kwa kulinganisha mambo mbalimbali ya kisheria wenzao Urusi wanayatatuaje katika harakati za kujiweka salama, kisheria na kiuchumi.
Amesema linalofanyika hapo ni kudumisha na kutekeleza falsafa ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika 4R kuna moja inayohusu jambo linalofanyika hapo leo, na kusema nchi lazima ishirikiane na nyingine ili kupata ushirika na uzoefu kutoka kwa wageni.
Dkt. Chana amesema mihadhara kama hiyo hufundisha wanafunzi wa fani mbalimbali na kuleta ufahamu na weledi katika masomo yao wanayofanya kwa vitendo kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.
“Urusi ni wazuri wa mambo ya Teknolojia katika ulinzi na usalama kisheria hivyo vijana hao wakipata kujifunza kutoka kwa Wataalam wataongeza ujuzi na kuutumia siku zijazo kwa manufaa yao na nchi yao” ameeleza Dkt. Pindi Chana.
Aidha, Dkt. Chana amesema wageni hao wametoka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Urusi kutembelea Tanzania kwa shughuli za kujifunza na kudumisha uhusiano na ushirikiano ulikuwepo hata kabla ya Uhuru nchini.
Mhadhara huo uliofunguliwa na Mhe. Pindi Chana umehudhuriwa na wanafunzi wa taasisi hiyo, wataalam kutoka Urusi na wageni mbalimbali waalikwa bila kusahau wahadhiri mahiri katika taasisi hiyo.