Wananchi wa Jimbo la Ilemela mkoa wa Mwanza wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa za El Nino zinazoendelea kunyeesha maeneo mbalimbali nchini ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo mafuriko na uharibifu wa miundombinu
Rai hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Ilemela MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni ambapo amewataka wananchi wa Igombe kata ya Bugogwa kuwa makini nyakati za mvua kwa kuhakikisha watoto hawazururi hovyo na kupita kwa umakini maeneo yote yenye madaraja ili kuepuka kusombwa na maji
‘.. Tumepita maeneo ya sangabuye mito yote imejaa maji na hata hapa Igombe tumekuta daraja limejaa maji kiasi cha kututaka tusubiri maji yaishe ili tuendelee na safari, kinachoendelea nchi nzima juu ya mvua kubwa kunyeesha na ilemela kipo, Rai yangu kwa wananchi pale zinaponyeesha mvua kubwa wasiwe na ujasiri wa kutaka kuvuka wasubirie mvua ikate ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula amemshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 66 kwa wakala wa barabara nchini TANROADS ili mvua zitakapokwisha miundombinu muhimu kama barabara na madaraja viweze kurejeshwa katika hali yake ya kawaida kufanya uwepo wa mawasiliano baina ya sehemu moja kwenda nyengine
Pauline Simon ni mkazi wa Igombe kata ya Bugogwa ambapo amemshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua huku akitaka viongozi wa ngazi za kata na mitaa kuiga mfano huo badala ya kusubiria maafa yatokee