Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kimeitaka Serikali ya wilaya hiyo kupitia wataalam wake wa maendeleo ya jamii kuweka utaratibu mwepesi na mifumo rahisi itakayowafanya wanawake wa wilaya hiyo kupitia vikundi vyao kuweza kuomba mikopo kwa njia ya kielektroniki kwa wepesi na bila urasimu.
Hayo yamesemwa na katibu wa ccm wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga wakati wa mkutano wa wanawake wajasiriamali uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Maliasili ambapo amewataka wataalam wa manispaa kuhakikisha wanawake na vikundi vyao wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya namna ya kuomba mikopo hiyo kupitia mfumo na kutowatisha au kuwawekea urasimu wa aina yeyote utakaokwamisha juhudi zao za kutaka kujikwamua kiuchumi
‘.. Watu hawana vishikwambi wala smartphone, hawajui kama siku hizi uombaji ni kwa njia ya mtandao, hamjawapa elimu ya kutosha tena wataalam wengine wanasahau kuwa familia zetu zina uelewa mdogo na nyie wa halmashauri wengi wenu mna digrii moja, mbili wengine mpaka tatu msizani wote tunafanana ..’ Alisema
Aidha Katibu Milanga amewataka wanawake hao kuendelea kuwaunga mkono viongozi wanawake wenzao akiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan, Mbunge Dkt Angeline Mabula na katibu tawala wilaya ya Ilemela Wakili Bi Mariam Msengi
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka wanawake hao kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa kutokukubali kukata tama juu ya kujifunza vitu vipya huku akiwaasa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwakaa huu na mwakani kwa nafasi za serikali za mitaa, udiwani na ubunge huku akiwaomba kuendelea kumuunga mkono Rais Mhe Dkt Samia katika nafasi ya Uraisi sanjari na kuwasisitiza kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura
Bi Peace Makungu ni miongoni mwa wanawake wajasiriamali waliohudhuria mkutano huo ambapo ametaka wanawake waelimishwe juu ya fursa zinazopatikana kupitia halmashauri huku Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wa CCM wilaya ya Ilemela UWT Bi Salome Kipondya akiwapongeza wanawake viongozi kwa kazi nzuri za maendeleo wanazozifanya na kusisitiza kuwa mwaka 2025 watawachagua tena katika nafasi zao za Urais na ubunge