Baadhi ya viongozi wa Chama cha watoa huduma Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wake Omari Chika wa kwanza kulia,wakimsikiliza Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro(hayupo pichani)wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya urasimishaji wa kazi za wasanii Waandishi wa Vitabu na ugawaji wa vitabu kwa shule zenye wanafunzi wa mahitaji maalum wa mkoa wa Ruvuma yaliyofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea jana.
……………………………
Na Mwandishi wetu
Songea
SERIKALI imewataka Wasanii,Waandishi wa vitabu na wabunifu wa Mkoani Ruvuma,kuhakikisha wanajisajili na kusajili kazi zao katika ofisi ya Hakimiliki Tanzania(COSOTA) ili waweze kunufaika na kazi zao pamoja na fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za fedha.
Wito huo umetolewa jana na Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro,wakati akifungua mafunzo ya urasimishaji wa kazi za Sanaa,uandishi na ugawaji wa vitabu na vifaa vya majaribio vya kusaidia kusoma kwa shule ya Msingi Luhira na St Vicent zilizopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Alisema,wakati umefika kwa wasanii wa mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla kuona umuhimu wa kurasimisha kazi zao ili zitambulike rasmi,huku akiwaagiza COSOTA na mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania kuwafikia wadau hao hasa waliopo katika mikoa ya pembezoni ili waweze kuwa na uelewa na faida ya urasimishaji wa kazi zao.
“urasimishaji una faida nyingi sana ikiwemo usimamizi wa kazi zenu kulindwa na sheria ya Hakimiliki na fursa ya za biashara kwa sababu mtatambulika na mtaweza kujiongezea kipato binafsi,familia na jamii kwa ujumla”alisema Dkt Ndumbaro.
Kwa mujibu wa Dkt Ndumbaro, kwa sasa sekta ya Sanaa na utamaduni inaongoza kwa ukuaji wa Uchumi kwa asilimia 19,hivyo wasanii ni lazima wahakikishe wanaongeza bidi katika kazi zao ili serikali nayo iweze kunufaika kutokana na kazi zao.
Amewataka kujitambua,kutambua thamani ya kazi zao,kuwa na nidhamu na kufanya kazi kwa weledi ili waweze kufanikiwa kwenye safari yao ya kisanii ndani na nje ya nchi.
Dkt Ndumbaro alisema,wilaya ya Songea na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ni chimbuko la utamaduni na Sanaa hapa nchini akiwemo Mrisho Mpoto,Joseph Haule(Frofesa J)Joseph Mbilinyi(Mr Sugu)Kosmas Chidumule na wengineo wanaotamba katika tasnia ya sanaa hapa nchini.
Alisema,licha ya mkoa huo kuwa na vijana wengi wenye vipaji,lakini wasanii wake wanashindwa kuonekana na kufanya vizuri Kitaifa na Kimataifa kutokana na kukosa ushirikiano baina ya wasanii na wadau licha ya Serikali kuweka mazingira mazuri kutambulisha kazi zao.
Afisa Mtendaji Mkuu na Msimizi wa Hakimiliki Tanzania Doreen Sinare alisema,mafunzo hayo yameambatana na utoaji wa vifaa vya majaribio kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wenye uoni hafifu kwa shule mbili za Luhira na St Vicent zilizopo katika Manispaa ya Songea.
Amewataka wasanii wenye vipaji kujisajili kupitia baraza la michezo ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali na taasisi mbalimbali za fedha.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya St Vecent Agnetha Mlelwa,ameishukuru serikali kupitia wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kutoa vifaa hivyo kwani vitasaidia wanafunzi wenye uhitaji kufanya vizuri katika masomo yao.